Mabadiliko ya mazingira ya ufanyaji biashara yanayoletwa na maendeleo ya uchumi wa viwanda pamoja na mnyororo wa thamani, yameelezwa kuwa changamoto kubwa katika jitihada za kuimarisha hali ya usalama na afya za wafanyakazi katika sehemu za kazi hapa nchini.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Eric Shitindi wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) leo mjini Dodoma.

Amesema kuwa mabadiliko hayo yanahusisha matumizi ya teknolojia za kisasa na ongezeko kubwa la idadi ya wafanyakazi katika sekta zote za umma na za binafsi jambo ambalo linahitaji utaalamu mkubwa katika kuweka na kusimamia mifumo ya kulinda afya na kuwahakikishia usalama wafanyakazi wote wanapokuwa katika sehemu zao za kazi.

“Hivyo mkiwa kama wataalamu katika masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi mnatakiwa kuwa na mikakati mipya ya kukabiliana na changamoto hizo. Hii itakuwa ni pamoja na kubadilika kifikra na kimtazamo katika utendaji kazi,” alisema Katibu mkuu Shitindi.

Aidha, Shitindi ameupongeza uongozi wa OSHA kwa mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa mpango kazi wake katika kipindi cha robo tatu za mwaka huu wa fedha (2016/2017) ambapo kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa katika baraza hilo, taasisi imevuka  malengo katika kaguzi, utoaji wa mafunzo ya usalama na afya kazini pamoja na huduma mbali mbali zitolewazo mahali pa kazi.

Hata hivyo, Katika hotuba yake ameahidi kuendelea kuisaidia OSHA kutatua changamoto zilizopo zikiwemo za kiutendaji na kuwaasa watumishi wa Wakala kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ikiwemo kuepuka kujihusisha na vitendo vya upokeaji rushwa wanapotekeleza majukumu yao.

 

Emre Aanika ndoto yake kwa Real Madrid na Barcelona
Live: Waziri wa Ethiopia, Rais Magufuli Ikulu Dar es salaam