Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amejitokeza kuchukua fomu ya kugombea Ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi katika jimbo la Kilosa na kuseama hagombei kutafuta umaarufu.

Amesema baada ya kulitumikia taifa kwa ujumla kupitia taaluma yake sasa ni wakati wa kushirikiana na wananchi wa Jimbo la Kilosa Mkoani Morogoro ili kutatua changamoto zinazowakabili kutokana na uzoefu wa kiutendaji alioupata.

Amesisitiza hakwenda jimboni humo kutafuta umaarufu bali kutatua changamoto mbalimbali hususani migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikisababisha mauaji pia kulifanya jimbo hilo kuwa eneo la kimkakati kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo na biashara na kuhamasisha uwekezaji ambao utatatua changamoto nyingine ikiwemo maji na barabara.

Jumla ya wanachama 19 wa Chama Cha Mapinduzi katika jimbo la Kilosa jana, wamejitokeza kuchukua fomu za kugombea Ubunge katika jimbo hilo ikiwa ni siku ya kwanza tu tangu zoezi la uchukuaji fomu kupitia CCM lianze rasmi.

Kaimu Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Kilosa, Filbert Kapenda amesema mwamko wa uchukuaji fomu za kugombea nafasi ya Ubunge kwa jimbo hilo la Kilosa ni kubwa na kwamba kwa hii leo pekee jumla ya wanachama 19 wamejitokeza kuchukua fomu kwa jimbo la Kilosa pekee huku jimbo la Mikumi wakiwa wamejitokeza wanachama 20.

Pazia la uchukuaji fomu kwaajili ya kugombea nafasi za udiwani na ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi kwa Tanzania Bara pamoja na Zanzibar kwa kiti cha uwakilishi linatarajiwa kuhitimishwa Julai 17,2020.

Mnyika hagombei Ubunge, kujenga chama kama Nyerere
Morisson apigwa "DANADANA" Young Africans