Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba ametoa siku 5 kwa viongozi wa Mkoa wa Rukwa kuhakikisha kuwa shughuli zote za kilimo na ufugaji zinazofanyika katika kingo za Ziwa Rukwa zimesitishwa.

Makamba alitoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Nankanga, Wilaya ya Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa  katika eneo la Forodhani lililoko ufukweni mwa Ziwa Rukwa.

Waziri Makamba alisema kuwa kutokana na shughuli za binadamu pamoja na mambo mengine, kina cha Ziwa hilo limepungua kwa takribani mita 3 katika kipindi cha miaka 16 ambapo mwaka 2000 kina hicho kilikuwa mita 6 na hivi sasa ni takribani mita 3 pekee.

Aidha, aliainisha kuwa Serikali itachukua hatua za muda mrefu kuhakikisha inaokoa ziwa hilo huku akiagiza kusitishwa kwa shughuli zote za kilimo ndani ya mita 60 za ukingo wa ziwa hilo kwa mujibu wa sheria ya mazingira, sheria ya maji na sheria ndogo ya serikali za mitaa kama sehemu ya hatua za awali za kuliokoa.

Aliongeza kuwa kuanzia Oktoba 28 ambapo siku tano alizotoa zitakuwa zimefikia ukomo, kusiwe na mtu yeyote anayejihusisha na shughuli za ufugaji au kulisha mifugo yake ndani ya mita 200 za ukingo wa ziwa hilo.

ufugaji

Katika hatua nyingine Waziri Makamba amesema Serikali itaagiza Halmashauri zote za Wilaya ambazo Ziwa Rukwa linapita kukusanya pesa kutoka katika vyanzo vyake ili ziweke alama (Beacon) na vibao katika mita 60 na Mita 200 kutoka kwenye hifadhi ya ziwa na kuujulisha umma kuwa hairuhusiwi kufanya shughuli katika maeneo husika.

Pia, Waziri Makamba alisema kuwa amebaini mkoa huo uko nyuma katika upandaji miti huku ukiwa na kiwango kikubwa cha utakati miti ya asili. Hivyo, aliagiza zoezi la upandaji miti kuanza mara moja.

Makamba anaendela kuzuru maeneo mbalimbali ya mikoani kupitia ziara yake mahsusi iliyolenga kuhamasisha utunzaji wa mazingira na anatarajia kuizuru mikoa mingine ikiwa ni pamoja na Katavi, Kigoma, Tabora na kuhitimisha ziara yake mkoani Dodoma.

 

 

Video: Waziri Mwijage asema watanzania wanapenda elimu 'mserereko', Azungumzia elimu yake
Lipumba awavaa Chadema, ‘mnajenga Ukuta wa biskuti..!’

Comments

comments