Mshindi wa tuzo za Oscar, Lupita Nyong’o ameanika maovu aliyofanyiwa na mtayarishaji nguli wa filamu za Hollywood, Harvey Weinstein ambaye amelalamikiwa na zaidi ya waigizaji 40 wa kike kwa vitendo hivyo.

Lupita ameanika uovu wa Harvey kupitia New York Times, ambapo ameeleza kuwa alifanyiwa vitendo hivyo akiwa chuoni akijaribu kutafuta namna ya kuingia kwenye mkondo mkuu wa filamu za Hollywood.

Nyota huyo wa 12-Years A Slave amesema kuwa alitambulishwa kwa Harvey na mwanamke mmoja ambaye alikuwa mdau mkubwa wa kiwanda cha filamu walipokutana katika hafla moja. Anasema mwanamke huyo alimwambia kuwa Harvey ni mtu muhimu sana kama anataka kufanikiwa kuigiza filamu kubwa zenye thamani ya mabilioni.

Hata hivyo, anasema mwanamke huyo baada ya kumtambulisha alimtahadharisha kuwa ingawa Harvey ni mtu mzuri kwenye biashara, anapaswa kukaa naye mbali kwenye maisha mengine.

Lupita anasema baada ya siku kadhaa Harvey alimualika nyumbani kwake kwa lengo la kuangalia filamu lakini mambo hayakuwa kama alivyotarajia.

“Nilikaa kwa ajili ya filamu, lakini baada ya dakika 15 Harvey alinifuata, aliniambia anataka kuniambia kitu. Alinipeleka hadi kwenye chumba chake cha kulala na akaniambia kuwa anataka kunipa ujumbe,” Lupita alisimulia.

“Kwanza, nilidhani anatania. Lakini alikuwa hatanii. Kwa mara ya kwanza tangu nikutane naye nilijisikia siko salama. Nilipaniki kidogo na nikafikiria kitu cha haraka cha kumtuliza ambacho kitanifanya niweze kumdhibiti kutotumia nguvu,” aliendelea.

“Alinikubalia, akalala kifudifudi na nikajifanya namtomasa mgongoni wakati naendelea kufikiria namponyoka vipi! Lakini kabla muda haujaenda aliniambia anataka kuvua nguo yake ya ndani. Nilimwambia asifanye hivyo kwa sababu sitaweza kuwa katika hali ya kawaida (confortable) hata kidogo. Hata hivyo, aliamka ili afanye hivyo. Na mimi niliamka na nikakimbilia kwenye mlango,” alifunguka zaidi.

Lupita anasema kuwa Harvey alijaribu kumshawishi tena kwa kumtajia majina ya waigizaji wawili wa kike wakubwa wa Hollywood ambao wamefanikiwa sana baada ya kumliwaza kitandani.

“Nilimwambia siko tayari kufanya hivyo na kwamba kama hatuendi kuangalia filamu mimi narudi shule,” alisema.

Muigizaji huyo ambaye alifanikiwa kuponyoka mikononi mwa Harvey usiku ule, alitaja tukio lingine kama hilo la jaribio la kumnyanyasa kingono lililofanywa na Harvey na kuwataka wanawake wengine ambao aliwatendea hayo kutokaa kimya na kuzungumza wazi.

 

Harvey anakaririwa na kashfa za unyanyasaji wa kingono na kuwasumbua wanawake kingono kwa kutumia mgongo wa nafasi yake ya utayarishaji wa filamu katika kiwanda cha Hollywood. 

Kizza Besigye asweka ndani na polisi
Dar, Geita, Kagera zang'ara matokeo darasa la saba

Comments

comments