Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amezungumzia tofauti iliyokuwepo kati yake na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu miaka kadhaa iliyopita, wakati wa vuguvugu lililomng’oa kwenye Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Zitto amekiri kuwa kulikuwa na ugomvi mkubwa kati yake na baadhi ya viongozi wa Chadema ikiwa ni pamoja na Lissu ambaye ni mwanasheria mkuu wa chama hicho, na kwamba walifikia hatua ya kutukanana.

Mwanasiasa huyo ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Chama Cha ACT – Wazalendo, amesema kuwa tofauti kati yao zilikuwepo kutokana na kupishana hoja na njia za kushindana na chama tawala (CCM), na kwamba tofauti hizo hazitaisha bali zinapaswa kutafutiwa utatuzi bila kuwepo ugomvi.

“Kwanza ni vizuri kufahamu kwamba tofauti hazitakaa ziishe. Binadamu wanapaswa kutafuta njia za kuweza kutatua tofauti zao bila kugombana,” Lissu aliiambia Kwanza TV.

Hata hivyo, Zitto ambaye amesema kuwa hivi sasa amekuwa karibu na Lissu zaidi ya wakati wowote ule, amekumbuka kauli ya Mbunge huyo wa Singida Mashariki alipomtembelea Ubelgiji alipokuwa akipatiwa matibabu, akionesha kujutia mikwaruzano isiyo na sababu kati yao.

“Nakumbuka siku moja nilivyoenda kumuona Lissu Ubelgiji na katika mazungumzo, moja ya jambo aliloniambia alisema, ‘muda huu nimekaa nje ya nyumbani kwenye matibabu kuna jambo moja ambalo nimelitafakari sana, tumemwaga sana damu zetu wenyewe bila sababu, kwangu yale yalikuwa maneno mazito sana,”alisema Zitto.

Zitto alisema kuwa ukaribu wake na Lissu kwa sasa umevuka mipaka ya wao pekee, bali umeziunganisha pia familia zao tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Lissu ambaye hivi sasa anaonekana akifanya ziara katika nchi mbalimbali ughaibuni, alipelekwa nchini Ubelgiji kwa ajili ya matibabu kufuatia tukio la kushambuliwa kwa risasi, Septemba 7, 2017 nyumbani kwake eneo la Area D jijini Dodoma.

Naibu waziri Ikupa ahimiza ushirikiano
Mama yake Godzilla ataka nyimbo za injili za mwanaye zichezwe msibani

Comments

comments