Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru), mkoani Rukwa imesema kuwa katika ufuatiliaji wake wamebaini jumla ya kaya 224 zisizo na sifa wilayani Nkasi zimepokea fedha za mfuko wa maendeleo ya jamii (Tasaf), awamu ya tatu kimakosa.

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Rukwa, Hamza Mwenda amebainisha zengwe hilo alipozungumza na waandishi wa habari katika taarifa yake ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo katika kipindi cha Octoba hadi Desemba 2018, huku akisisitiza kuwa huo ni mwanya wa upotevu wa fedha za Serikali.

Amesema kuwa katika kipindi hicho taasisi hiyo ilipokea taarifa kuwa maofisa watendaji wa kata wilayani Nkasi wamekuwa wakikusanya fedha kutoka kwa kata zilizopata fedha za Tasaf awamu ya tatu bila kuwa na sifa huku ikiwa haieleweki fedha hizo zilipelekwa wapi.

“Nikweli kuwa halmashauri ya wilaya ya Nkasi iliagiza maofisa watendaji wa kata wasimamie urejeshwaji wa fedha hizo lakini tumebaini kuwa zoezi hilo halikuwekewa utaratibu na halmashauri, huu ni mwanya wa upotevu wa fedha za serikali,” Mwenda amebainisha

Hadi sasa ofisi ya Tasaf wilaya ya Nkasi na Halmashauri ya wilaya hawafahamu kiasi cha fedha kilichokusanywa na pia hakuna maelekezo ya wapi fedha zilizokusanywa ziwasilishwe, kwani fedha hizo zilikuwa zinapokelewa bila kumbukumbu yeyote ya maandishi.

Aliongeza kuwa kufuatia kuwepo kwa mwanya huo ambao unaweza kusababisha upotevu mkubwa wa fedha za serikali, Takukuru imeafikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi na Tasaf kuwa Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji  ya Halmashauri ihakikishe fedha zinazokusanywa zinawasilishwa wilayani NA hatimaye Tasaf Makao Makuu

Aidha, amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kuandaa utaratibu wa kutunza kumbukumbu za mrejesho wa fedha hizo, na kwamba taasisi hiyo itaendelea kufuatilia suala hilo mpaka hapo litakapo kamilika.

Tasaf awamu ya tatu imelenga katika makundi maalumu ya watu maskini ili waweze kupiga hatua kubwa ya maendeleo na kujitegemea kwa kupambana na umaskini.

Wanaopewa nafasi kubwa katika awamu hiyo ni wazazi na walezi kwa ajili ya kusomesha watoto wao na kutumia kama fursa ya kupata matibabu.

Anusurika kifo kisa marejesho ya mkopo
Familia yapoteza watoto watano kwa kula samaki wenye Sumu