Kocha mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, Zeben Hernandez, amekiweka sawa kikosi chake kukabiliana na kila hali katika mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Ndanda utakaofanyika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara Jumamosi ijayo (Septemba 24, 2016).

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na lengo moja tu la kuhakikisha inaibuka na ushindi kutokana na kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Simba (1-0) licha ya kuonyesha kiwango bora kwa asilimia kubwa ya mechi hiyo.

Zeben ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mapema leo mara baada ya mazoezi ya asubuhi kuwa anajua aina ya uwanja anaoenda kuuchezea huku akisema amekipanga kikosi chake kufanya vizuri na kwa kushinda kipute hicho.

“Tutabadilisha aina yetu ya mpira kwa sababu uwanja tutakaochezea ni mbaya sana, tunauchukulia kwa uzito mkubwa sana mchezo huo, tutacheza soka la mipira mirefu sana lakini kwa urahisi, hili ni jambo la muhimu sana kutokana na aina ya uwanja tutakaochezea,” alisema.

Ili kuonyesha amepania kukabiliana na uwanja huo pamoja na wapinzani wake, Kocha huyo raia wa Hispania kwa siku mbili hizi tokea jana hadi kesho asubuhi, amekuwa akikipika kikosi chake katika uwanja wa nyasi za kawaida unaoendana kidogo na Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Zeben alisema kuwa jambo la muhimu kwa leo na kesho ni baadhi ya wachezaji waliocheza mchezo uliopita kufanya mazoezi ya kurudisha miili yao vizuri kabla ya kuamua kikosi kitakachokwenda kuikabili Ndanda, kitakachosafiri kesho Alhamisi mchana.

“Kwangu mimi mchezo uliopita (Simba) ulikuwa mzuri kwa timu yangu, tulikuwa bora mchezoni zaidi ya Simba, lakini kwa kosa moja tulilolifanya Simba waliweza kulitumia na kufunga bao, kwa sasa ninachofanya ni kuwaweka sawa wachezaji wangu na muhimu kwangu kwa sasa ni kuweka akili yetu kwa mchezo ujao na kuachana na habari za mchezo uliopita,” alisema.

Mpaka sasa katika msimamo wa ligi hiyo hadi raundi ya tano inamalizika, Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB na kinywaji safi cha Azam Cola kinachosisimua koo, inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa na pointi 10 sawa na Yanga iliyo nafasi ya pili huku Simba ikiwa kileleni kwa pointi 13 ilizojikusanyia.

Picha 23: Majaliwa azindua mpango mkakati, mradi wa maboresho ya Mahakama Tanzania
Picha: Kilimanjaro Queens Yawasili Nchini Kupitia Kagera