Siku chache baada ya kuibuka kwa sakata la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kutangaza kukata umeme kwa wadaiwa sugu, likiwemo Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepata matumaini ya kuwa na umeme wa uhakika.
 Matumaini hayo ya Zanzibar kuondokana na tatizo la umeme wa kutegemea sehemu moja yameanza kuonekana baada ya utafiti wa nishati mbadala unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) kuonyesha uwezekano wa rasilimali hiyo kupatikana bila ya matatizo visiwani humo.
Akizungumza katika ziara iliyofanyika jana kwenye vituo vya utafiti wa uzalishaji umeme wa upepo na nishati ya jua mikoa ya Zanzibar, Meneja wa mradi huo, Munir Shirazi Hassan amesema utafiti ulioanza mwaka 2016 kwa ufadhili wa EU unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili na kufuatiwa na ushauri yakinifu kutoka kwa wataalamu.
 “Tunasubiri kwa hamu huduma hii ianze kutumika, tunadhani kufanikiwa kwake kutasaidia kushuka kiwango cha matumizi ya umeme kutoka Tanesco kwa zaidi ya asilimia 50 ili kuondokana na deni la matumizi ya kila mwezi.”amesema Munir.
Aidha, Ofisa mawasiliano kutoka Kampuni ya Ubelgiji, Sebastian Sanga amesema  kukamilika kwa mradi huo kutaiondolea Zanzibar adha ya kutegemea umeme kutoka sehemu moja.
Hata hivyo, Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar imeshaanza kulipa deni la Tanesco, huku shirika hilo likiendelea na operesheni yake ya kuwakatia umeme wadaiwa wote sugu.

Rand ya Afrika Kusini yazidi kuporomoka kwa kasi
Video: Ikulu yamtwisha 'mzigo' Waziri, Wizi mkubwa Dar