Mtangazaji mahiri aliyetikisa na kipindi cha Take One ya Clouds TV, Zamaradi Mketema amewajibu waliodai kuwa baadhi ya jumbe zake kwenye Instagram zinatokana na kuwa na msongo wa mawazo(stress) unaohusishwa na maisha ya mapenzi.

Zamaradi ambaye mwaka jana alikuwa miongoni mwa watu waliohusika kwenye matukio yaliyozua gumzo (most trending) kwenye mitandao ya kijamii baada ya kufunga ndoa na Shabani ambaye wengi hawakuwa wanamtarajia au kumfahamu, amesema kuwa anachokiandika kwenye Instagram ni mawazo yake binafsi kuhusu maisha kwa lengo la kuwasaidia watu wengine na sio vinginevyo.

Mtangazaji huyo ambaye ni mama wa watoto wawili wa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba alifunga ndoa iliyofuatiwa na sauti iliyovuja mitandaoni iliyoaminika kuwa ni ya Ruge akimlilia kuhusu uamuzi aliouchukua.

Akifunguka hivi karibuni kupitia ‘Chill na Sky’, mtangazaji huyo amesema kuwa kutokana na anachokiandika, amekuwa akipata jumbe nyingi za watu wanaotaka awashauri hususan kuhusu masuala ya mahusiano ya mapenzi na amekuwa akifanya hivyo na kuona matunda.

“Nikishaona suala la mtu ni zito nampa namba ya simu tunawasiliana namshauri. Na wamekuwa wakinipigia simu kunieleza maendeleo na wananishukuru. Hicho kwangu ni kitu kikubwa sana,” alifunguka.

Alieleza kuwa amekuwa akipokea simu za watu ‘wakubwa’ ambao wanamuuliza mwingine kama anachokiandika huwa anaki-google au ni mawazo yake binafsi, hali inayomfanya aone ukubwa wa maandishi yanayotokana na fikra zake binafsi.

Amesema anaendelea na mpango wake wa kuyakusanya anayoyaandika na kuandaa kitabu ili kutimiza ahadi aliyowapa mashabiki wake muda mrefu.

Hata hivyo, Zamaradi amedai kuwa kuna wakati alikuwa anashindwa kuandika vitu ambavyo anavifikiria kwa sababu aliamini akiandika hivyo watu wanahusisha na matukio yanayoendelea yanayomhusu, lakini sasa ameona hakuna haja ya kufikiria nani anawaza nini ili mradi ana kitu kizuri kwa jamii.

Zamaradi ambaye alikiinua kipindi cha ‘Take One’ cha Clouds TV na kushiriki uandaaji wa filamu maarufu kama ‘Kigodolo’ na nyingine amesema kuwa hakuna anachojutia kwenye maisha yake na kwamba aliyefunga naye ndoa ni mtu anayemfahamu vizuri tofauti na baadhi ya watu wanavyofikiria.

Amesema kutokana na kiu ya watu kuhitaji arejee kwenye utangazaji, atarejea tena kwa kishindo kwani yeye na Clouds Media Group hakuna ambaye amemuacha mwenzake na ndio sababu bado akaunti yake ya Instagram inamtambulisha kama mwanafamilia wa kituo hicho cha habari.

Waziri Mwakyembe atembelea Serengeti Boys
Mpina awataka wafugaji kupaza sauti