Wachezaji saba wa Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wataukosa mchezo wa kesho unaotarajiwa kuchezwa dhidi ya Azam FC katika dimba la Azam Complex kutokana na sababu mbalimbali walizokuwa nazo.

Hayo yamesemwa hii leo jijini Dar es salaam na Afisa Habari wa klabu hiyo, Dismas Ten ambapo amewataja wachezaji kuwa ni Yohana Mkomola, Thaban Kamusoko, Amisi Tambwe, Abdallah Shaibu, Donald Ngoma pamoja na Pato ngonyani ambao wote ni majeruhi huku Pius Buswita akiwa anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano alizozipata katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Azam FC ni wachezaji saba pekee ndio watakaokosa mchezo huo kama nilivyosema lakini kila kitu kimekamilika. Tunaiheshimu sana Azam kwani wamekuwa na msimu mzuri wanapata matokeo ndani na nje ya uwanja wao wa nyumbani ila ata sisi Yanga SC tupo vizuri na tunatarajia kupata matokeo kwenye mchezo wa kesho,”amesema Ten

Hata hivyo, Azam FC kesho itakuwa inaikaribisha Yanga SC katika dimba lao la nyumbani ambapo mchezo huo utachezwa majira ya 10:00 alasiri kwa saa za Afrika Mashariki.

Video: Dkt. Ndugulile ahimiza mapambano dhidi ya Ukoma
Ruby: Niliamua kuomba msamaha, Ruge Mutahaba ni kama baba yangu