Wagonga nyundo wa jijini London, West Ham Utd, wamewashiwa taa ya kijani kumsajili moja kwa moja kiungo kutoka nchini Cameroon, Alexandre Dimitri Song Billong baada ya kuridhishwa na uwezo wake.

Muwekezaji mwenza wa klabu hiyo ya magharibi mwa jijini London, David Sullivan amethibitisha kufanyika kwa mazungumzo kati yake na viongozi wa FC Barcelona ambao walikubali kumpeleka Song kwa mkopo huko Upton Park msimu uliopita.

Sullivan, amesema kiungo huyo mwenye umri wa miaka 27, atasaini mkataba wa miaka mitatu endapo atafanikiwa kupita kwenye vipimo vya afya ambavyo anatarajiwa kufanyiwa hii leo.

Tajiri huyo kutoka nchini Wales amesema, Song analazimika kufanyiwa vipimo vya afya kwa ajili ya kufahamu utimamu wake wa mwili, ambao unatakiwa kuendana na vigezo vilivyowekwa klabuni hapo.

Song, alikua mchezaji wa klabu ya Arsenal kuanzia mwaka 2006–2012, kabla ya kuuzwa kwenye klabu ya Barcelona ambapo alikaa Camp Nou kwa miaka miwili kabla ya kupelekwa kwa mkopo Upton Park, msimu wa 2014-15.

Otamendi Kujimilikisha Man City
Wawili Hawa Kuihama Southampton