Msanii wa filamu na mwanamitindo nchini, Jackline Wolper amejikuta akiwaombea msamaha mtangazaji wa kipindi cha Shilawadu Soudy Brown na Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Maua Sama wanaoshikiliwa na jeshi la polisi siku ya tano sasa kwa kosa la uharibifu wa mali za umma.

Wolper ametumia ukurasa wake wa instagram kuwaomba viongozi wakubwa kuwasamehe wawili hao kwani walikuwa katika harakati za kutafuta pesa na kusisitiza kuwa adhabu hiyo waliyoipata inawatosha na iwe funzo kwa wengine.

“Katika utafutaji Kuna mitihani mingi Sana. Nachoweza kusema Nikuomba Tuu wakubwa muwasamehe vijana wenzetu Naamini katika Hili lililotokea Basi wengine wengi watajifunza kitu kupitia hili Naomba niwaombee masamaha wa Dhati kabisa Ndugu zetu Na wawe huru kuendelea Na majukumu yao inshallah. Maua & Soudy na wengine wore mliopo Ndani Juu ya hili sio sawa kutaja wote lakini hawa niwawakilishi poleni saanaa Jamani Ndani sio kuzuri,“ameandika Wolper.

Maua Sama na Soudy Brown walishikiliwa na jeshi la polisi tangu Septemba 16, mwaka huu mara baada ya kuposti video mbalimbali katika mtandao wa kijamii iliyowaonyesha wakicheza wimbo wa Iokote wa msanii huyo huku wakikanyaga noti za Sh.10,000.

Aidha Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Lazaro Mambosasa amesema uchunguzi zaidi unaendelea na endapo watuhumiwa hao watabainika kutenda kosa hilo watafikishwa mahakamani na kusisitiza kuwa ni kosa kisheria kwa mtu yeyote kuchezea fedha ya kitanzania.

 

Blogu yamtia mbaroni Shafii Dauda na wengine 7
Video: Soudy Brown, Maua Sama wasota rumande, Chadema hawaaminiki