Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Sekta ya Ujenzi imepongezwa kwa kupeleka fedha za kutosha kulingana na bajeti iliyoidhinishwa kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), ili kumuwezesha wakala huyo kutimiza majukumu yake.

Pongezi hizo zimetolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu chini ya Mwenyekiti wake Selemani Kakoso Jijini Dodoma mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Wakala huyo.

“Tayari mmepewa fedha za kutosha sasa kinachofuata ni kufanya kazi maana hatuhitaji mipango mizuri ya makaratasi bali tunataka vitendo kwa kutimiza wajibu kwa kile kilichokusudiwa na kufikia malengo”, amesisitiza Kakoso.

Mwenyekiti huyo pia ameitaka Wizara ya Ujenzi kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango ili kuhakikisha inasimamia kulipwa kwa wakati madai ya kiasi cha zaidi ya Shilingi Bilioni 31 ambazo wakala huyo anazidai taasisi za Serikali na Wizara. 

Kakoso ameongeza kuwa Wizara pia inatakiwa kuangalia namna bora ya kupunguza gharama za ununuzi wa magari pamoja na vipuri vyake ili kuweza kuipunguzia Serikali mrundikano wa gharama zisizo na ulazima.

Awali Naibu Waziri wa Ujenzi Elias Kwandikwa  amewaambia wajumbe wa kamati hiyo kuwa TEMESA ilifanikiwa kukusanya mapato ya kiasi cha zaidi ya shilingi Bili 58 kutoka vyanzo vyake vya ndani vya mapato na ruzuku ya Serikali kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2018/19.

“Fedha hizo ni kutoka katika vyanzo vya mapato vya ndani na hata hivyo katika mwaka huu wa fedha 2019/20 Wakala unatarajia kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 89 na tuna imani ya kufanya vizuri,” ameongeza Kwandikwa.

Amesema wakala umeanzisha karakana katika ngazi ya wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro ili kuhakikisha huduma inasogezwa karibu na wateja na kwamba tayari umenunua vitendea kazi vya kisasa ikiwemo gari lenye karakana (Mobile Workshop) ambalo litatoa huduma popote.

“Gari hili maalum litatoa huduma eneo lolote na kwa wakati wowote na pia wakala tayari umekamalisha ukarabati wa karakana za mkoa wa Singida, mkoa wa Dar es Salaam na mkoa wa Mwanza,” amefafanua Naibu Waziri huyo wa Ujenzi.

Kwa upande wake Mbunge wa Misungwi Charles Kitwanga amesisitiza umuhimu wa kuzingatia usalama wa abiria na mizigo katika vivuko kwa kuweka mifumo madhubuti ya kuonesha idadi kamili ya abiria na uzito wa mizigo ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.

Kikao hicho cha kamati kimeshirikisha wajumbe mbalimbali akiwemo Naibu Waziri wa Sekta ya Ujenzi Elias Kwandikwa, Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye na Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi Arch. Elius Mwakalinga ambapo taarifa ya utekelezaji ya TEMESA inayotokana na maazimio ya vikao vya Bunge vilivyopita ilijadiliwa na tayari imepokelewa.

Video: INAUMIZA! Baada ya kukatwa Ulimi, Saratani yatoboa Shingo | Chakula kinatoka| Mkewe aomba msaada
Serikali yapiga marufuku uuzaji nyama pori