Mkufunzi na mmiliki wa klabu ya  Arsenal, Arsene Wenger amethibitisha kuachana na timu hiyo mwisho wa msimu huu mara baada ya kuitumikia kwa muda wa miaka 22 na kuipatia mafanikio mengi timu hiyo.

Mapema leo hii Wenger amefanya mazungumzo na uongozi wa timu hayo na kufikia makubaliano hayo na kusema huu ni wakati wake muafaka kujiuzulu.

”Baada ya kutafakari na kufanya mazungumzo na klabu , nahisi ndio wakati muafaka kujiuzulu mwisho wa msimu huu. Nashukuru kwa kupata fursa ya kuihudumia klabu hii kwa miaka mingi. Niliongoza klabu hii na moyo wangu wote pamoja na maadili. Nataka kushukuru wafanyakazi, wachezaji Mkurugenzi na mashabiki ambao wameifanya klabu hii kuwa maalum. Nawaomba mashabiki wetu kuisaidia timu hii kumaliza msimu huu vizuri. Kwa wapendwa wote wa Arsenal tunzeni maadili ya klabu hii”. Amesema Arsene Wenger.

Wenger alimalizia kwa kutoa ujumbe akidai kuwa ataishabikia timu hiyo maisha yake yote.

Wenger mwenye umri wa miaka 68 alianza kuifundisha Arsenal Oktoba 1, 1996 na amefanikiwa kuipa mafanikio mengi tofauti tofauti ikiwemo rekodi ya kutwaa ubingwa wa EPL bila kufungwa mwaka 2003 pamoja na kutwaa ubingwa wa EPL mara tatu na Ubingwa wa FA mara saba.

Wenger ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu anaweza kuondoka akiwa ametwaa ubingwa wa Europa League ambapo yupo nusu fainali na atacheza na Ateltico Madrid.

EXCLUSIVE: Ukimkuta Mume/mke wako ana 'KISIMBUSI' utafanyaje? | Penyenye (S02E01)
Comey adai Trump hashauriki