Muigizaji wa kike na Miss Tanzania 2006, Wema Abraham Sepetu amezua tafrani katika Mkoa Singida kufuatia uamuzi wake wa kugombea ubunge wa viti maalum kupitia CCM, hali iliyopelekea Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake CCM (UWT) Wilaya ya Ikungi, Bi. Christina Hamisi kutishia kukihama chama hicho.

Bi. Christina alieleza kuwa amefikia uamuzi wa kutaka kukihama chama hicho na kujiunga na Chadema kwa sababu amekuwa akipokea vitisho kutoka kwa baadhi ya viongozi wa chama hicho ngazi za wilaya na mkoa kutokana na msimamo wake wa kutomuunga mkono Wema Sepetu.

Alieleza kuwa tangu mchakato huo uanze, amekuwa akipokea pia vitisho na lugha za matusi kutoka kwa watu wa karibu wa Wema akiwemo mama yake Mariam Sepetu lakini alipofikisha malalamiko yake kwa viongozi hao alipewa kauli za vitisho na kupuuzwa.

Alibainisha kuwa kutokana na tatizo hilo, aliamua kumfikishia malalamiko yake Katibu wa CCM wilaya ya Ikungi, Aluu Segamba lakini katibu huyo alimtaka aachane na habari hizo kwa kuwa mgombea huyo alipelekwa mkoani hapo na vigogo ambao ni viongozi wa ngazi za juu katika chama hicho wenye nyadhifa serikalini.

“Nimemweleza Katibu wa Wilaya mambo ninayofanyiwa, likini niliishia kuambiwa siwezi kupata msaada wowote kwenye ofisi hiyo na kwamba niachane na Wema kwa sababu ameletwa na kiongozi mmoja mkubwa wa serikali, mawaziri na mtoto wa kigogo agombee ubunge hapa,” alieleza Bi. Christina.

Mama yake Wema, Mariam Sepetu alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo alieleza kuwa hawezi kuongea chochote kuhusu Mwenyekiti huyo wa UWT Wilaya ya Ikungi.

Bi. Christina aliongeza kuwa baada ya kuona malalamiko yake hayafanyiwi kazi katika ngazi hizo, aliamua kumfikishia Katibu wa UWT wilaya ya Singida, Bi. Anjela Mirembe. Hata hivyo, Mirembe alipoulizwa, alikiri kuwa Bi. Christina alimfikishia malalamiko yake kwa njia ya mdomo badala ya maandishi kama zinavyoeleza taratibu za kiutendaji.

 

Kagame Cup Yaivuruga Yanga
Wamarekani Washambuliwa Kwa Risasi Katika Ukumbi Wa Sinema