Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga ametangaza kiama kwa wafanyabiashara wa mbegu nchini wanaouza mbegu feki zilizopigwa marufuku na Serikali.

Ametoa agizo hilo akiwa ziarani Mkoani Morogoro ambapo pamoja na mambo mengine alitembelea Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Taasisi iliyopewa jukumu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la usajili wa wafanyabiashara wa mbegu (Seed Dealers).

Hasunga amewataka wafanyabiashara wote wa mbegu ambao wamekuwa wakifanya biashara hiyo kwa kuwauzia wakulima mbegu feki zilizopigwa marufuku na Serikali kuacha haraka iwezekanavyo kwani Serikali itawachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kukiuka maagizo ya Serikali.

“Serikali imepokea malalamiko mengi kwa wananchi kuhusu Ubovu wa mbegu jambo ambalo limepelekea kwa kiasi kikubwa kuwa na mavuno kidogo pasina kukidhi matakwa ya wakulima wetu nchini” Amesema Hasunga.

Waziri huyo pia ameiagiza Taasisi ya udhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) kutimiza majukumu yao kwa kuwabaini wafanyabiashara wanaokiuka maagizo ya Serikali pamoja na taratibu na sheria za nchi.

“Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu mbegu feki jambo hili Serikali haiwezi kukubaliana nalo hivyo TOSCI wanapaswa kusimamia kwa weledi ukaguzi na usajili wa Mbegu bora, pia ni lazima kuwabaini wasambazaji feki wa mbegu ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao” Amesisitiza Mhe Hasunga

Ameeleza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa inaongeza thamani ya mazao yote yanayozalishwa nchini, sambamba na kutafuta masoko mazuri.

Aidha, ameitaja Wizara ya Kilimo kuwa ina wataalamu wengi hivyo unaandaliwa mfumo mzuri wa kuwaunganisha watalaamu hao ili kujadili kwa pamoja namna ambavyo kilimo kinaweza kubadilika kutoka kilimo cha kujikimu na kuwa kilimo cha kibiashara ili kutoa malighafi za kutosha zitakazohuisha serikali ya viwanda.Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akikagua Maabara ya Kutazama kiwango cha Uotaji wa Mbegu wakati wa ziara yake ya kikazi Mkoani Morogoro alipotembelea Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI). 

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akikagua shamba la mahindi wakati wa ziara yake ya kikazi Mkoani Morogoro alipotembelea Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI).
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Patrick Ngwediagi akitoa taarifa ya Taasisi hiyo mbele ya Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga.
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akikagua bustani ya nyanya wakati wa ziara yake ya kikazi Mkoani Morogoro alipotembelea Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI).

Walimu wapoteza maisha kwa ajali ya gari
Rais wa Zimbabwe azungumzia afya ya Mugabe, ‘hatembei’