Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Dessalegn anatarajiwa kuwasili nchini kesho, Machi 31 kwa ziara ya kitaifa ya siku mbili kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Hayo yamesemwa mapema hii leo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano Afrika Masharika, Dkt. Suzan Kolimba alipokuwa Akizungumza na waandishi wa habari, amesema kuwa ziara ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Dessalegn imetokana na mkutano kati yake na Rais Dkt. Magufuli uliofanyika baada ya mkutano wa kawaida wa 28 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika hivi karibuni huko nchini Ethiopia.

Amesema kuwa madhumuni ya ziara hiyo ni pamoja na kukuza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Tanzania na Ethiopia pamoja ‎na kujadili fursa zaidi za ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwemo uwekezaji na biashara.

“Mahusiano ya Tanzania na Ethiopia ni mazuri, Ethiopia imeonesha nia ya kufungua Ubalozi wake hapa nchini hivi karibuni. Kwa sasa Ethiopia inawakilishwa nchini na Balozi wake aliyepo Nairobi nchini Kenya” amesema Naibu Waziri Kolimba.

Wakati wa ziara hiyo,Waziri Mkuu wa Ethiopia, Dessalegn atakutana na Rais Dkt. John Magufuli kwa mazungumzo, watashuhudia uwekwaji saini wa mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali kabla ya kuzungumza na Waandishi wa Habari.

Aprili 01 mwaka huu, Waziri mkuu huyo wa Ethiopia atatembelea Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa Bandarini hapo, Dessalegn na ujumbe wake wataondoka siku hiyo hiyo kurejea Ethiopia.

Hata hivyo, Mwaka 2015 Waziri Mkuu wa Ethiopia, Dessalegn alitembelea Tanzania na kushiriki uzinduzi wa Kiwanda cha kutengeneza dawa za kuua viluwi luwi vya mbu wanaoeneza Malaria kilichojengwa Kibaha, Pwani kwa ufadhili wa Serikali ya Cuba.

#Hapokale
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (KJCI) yatoa neno kwa Rais Magufuli