Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka watalii kutoka Israel wakawe mabalozi wazuri wa kuitangaza Tanzania pindi wakirudi huko kwao.

Ametoa wito huo kwenye uwanja wa ndege wa Kilimanjaro (KIA) wakati akiwaaga watalii 274 walioondoka nchini kurejea kwao.

Watalii hao ni miongoni mwa watalii 1,000 waliowasili nchini tangu Aprili 20, mwaka huu na kutembelea maeneo kadhaa ya vivutio kwenye ukanda wa Kaskazini.

Majaliwa amewaomba watalii hao wapange muda wao na watafute fursa nyingine ya kuja Tanzania kutembelea mbuga nyingine za ukanda wa Kusini pamoja fukwe nzuri za Zanzibar.

“Tumefarijika sana na ujio wenu na tunaamini mtaenda kutangaza mazuri mliyoyaona kwa wengine. tunazo mbuga nyingine za Rubondo, Katavi, Ngorongoro, Ruaha, Selous, fukwe nzuri za Zanzibar na mlima Kilimanjaro,” amesema Majaliwa

Pia amewashukuru mawakala wa utalii nchini pamoja na Mkurugenzi wa kampuni wakala wa utalii ya Another World kutoka Israel, Carmel Shlomo kwa kuamua kuitangaza Tanzania kama kivutio namba moja cha utalii barani Afrika.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla amewashukuru watalii hao kwa kuamua kuitembelea Tanzania licha ya kuwa wangeweza kwenda maeneo mengine yaliyo jirani na Israel.

“Natambua uchovu mlionao sababu ya urefu wa safari kutoka Israel hadi hapa, lakini nawashukuru kwa uamuzi wenu wa kuja Tanzania katika kipindi hiki ambacho tunafanya maboresho kwenye sekta ya utalii ili tuweze kutoa huduma bora zaidi,” amesema Kigwangalla

Pia amezishukuru kampuni za Utalii za Tanzania na Israeli kwa kushirikiana kuleta watalii wengi kiasi hicho. ambapo amezitaja kampuni hizo kuwa ni Excellent Guides, Mauly Tours and Safaris, Matembezi, Leopard Tours and Safaris, African Queen Adventures na TAWISA zote za kutoka Tanzania. Kampuni za kutoka Israeli ni Another World, My Trip, Camel na Safari Company.

Kwa upande wao, baadhi ya watalii kutoka Israel wamesema kuwa wamevutiwa na waliyaona hapa nchini na wameahidi kurudi tena ili watembelee vivutio vingine zaidi.

 

 

Waokoaji wapata mtihani kwenye vijiji vilivyokumbwa na Kimbunga
Rais Magufuli atoa siku saba kwa wakuu wa mikoa inayodharisha dhahabu