Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amepokea msaada wa sh. milioni 121.679 ili kusaidia wananchi waliothirika na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera, Jumamosi, Septemba 10, 2016 na kusababisha vifo vya watu 17.

Majaliwa amepokea msaada huo katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma leo Septemba 16, 2016 kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo Meneja Rasilimali Watu wa Kampuni ya Caspian, Omid Karambech aliyetoa sh. milioni 100, wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bordar Limited, Wu Yahui aliyetoa sh. milioni 20 pamoja na Bi. Mariam Kitembe aliyetoa sh. milioni 1.679 kwa niaba ya Wauguzi walioshiriki mafunzo ya Utafiti wa viashiria na matokeo ya ukimwi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Majaliwa amewashukuru kwa michango yao ya fedha na kuwaomba wananchi wengine wajitokeze kwa wingi ili kuwasaidia watu walioathirika na tetemeko hilo ambalo ni kubwa na halijawahi kutokea nchini.

Tetemeko la ardhi lililotokea Kagera mbali na kusababisha vifo, watu wengine 253 walijeruhiwa na maelfu ya wananchi walikosa makazi baada ya nyumba 840 kuanguka na nyingine 1,264 zikipata nyufa yakiwemo majengo 44 ya taasisi mbalimbali za umma.

Waziri Mkuu alifanya ziara mkoani Kagera jumapili, Septemba 11, 2016, kuwapa pole waathirika wa tetemeko hilo pamoja na kujionea madhara yaliyojitokeza ambapo pia aliongoza maelfu ya wananchi wa Manispaa ya Bukoba kuaga miili ya watu 16 waliofariki kutokana na tetemeko hilo. Aliwaomba wananchi wawe watulivu na kuwaahidi kuwa Serikali itakuwa pamoja nao.

Jumanne, Septemba 13 mwaka huu Waziri Mkuu aliongoza harambee ya kuchangia waathirika wa teteme hilo na kupokea zaidi ya sh. bilioni 1.4 kutoka kwa mabalozi wa nchi za nje nchini Tanzania na Jumuia ya Wafanyabiashara wa Kitanzania.

 

Mshike Mshike Wa Ligi Kuu Bara Kuendelea Tena Kesho
Majaliwa - Uchumi wetu ni Shwari kabisa, Atoa hofu Watanzania