Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameishukuru Serikali ya China kwa kuunga mkono jitihada za maendeleo zinazofanyika nchini hivi sasa chini ya uongozi wa Serikali ya awamu ya tano.

Majaliwa ametoa shukrani hizo alipokutana na Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Watu wa China, Bw. Cai Dafeng ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.

“Tunaishukuru Serikali ya China kwa sababu tumepokea misaada na mikopo ya gharama nafuu na kuendeleza miradi mbalimbali kama vile mradi wa umeme wa Kinyerezi, awamu ya pili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Zanzibar,” amesema.

Amesema Serikali ya China imekuwa pia na mahusiano ya muda mrefu na Serikali ya Tanzania na hasa kwenye sekta ya afya ambapo kuna wanafunzi wengi wa Kitanzania ambao wako China wakisomea udaktari na masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).

“Tuna mahusiano mazuri kwenye sekta ya afya na sasa hivi tuna madaktari 20 ambao wanasoma huko na wengine wanasomea masuala ya TEHAMA. Pia tuna mahusiano mazuri baina ya Bunge la Tanzania na China,” amesema.

Waziri alisema Tanzania imejipanga kuinua uchumi wake kupitia ujenzi wa viwanda na sekta nyingine kama utalii kutokana na vivutio vilivyopo nchini kama vile Mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama za Serengeti na visiwa vya Zanzibar. “Nimefurahi kusikia kuwa hivi karibuni tutapata idadi kubwa ya watalii kutoka China,” amesema.

Akizungumza Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Watu wa China, Bw. Cai Dafeng alisema amefurahishwa na jinsi Serikali ya awamu ya tano inavyoendelea kubadili hali ya uchumi wa nchi na maisha ya Watanzania chini ya uongozi wa Dkt. John Pombe Magufuli.

Amesema China itaendelea kuiunga mkono Tanzania kwenye masuala ya kiuchumi na haiko tayari kuona ikiingiliwa masuala yake ya ndani na mataifa kutoka nje.

Kuhusu masuala ya uwekezaji baina ya Tanzania na China, Bw. Cai amesema China itaendelea kuyahimiza makampuni ya nchi hiyo ili yawekeze zaidi nchini Tanzania kwenye maeneo mbalimbali kama vile ujenzi wa bandari ya Bagamoyo. “China inataraji kuongeza uwekezaji kwenye kilimo, nishati na miundombinu,” amesema.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Novemba 18, 2018
Vijana ambao hawajaoa kuanza kulipa kodi