Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amekanusha taarifa zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa shule na vyuo vitafunguliwa Jumatano.

Taarifa hizo ambazo hazikuonesha chanzo chake, zilieleza kuwa Serikali imeagiza shule na vyuo kufunguliwa Jumatano, bila kueleza ni Jumatano ipi.

“Hizo ni taarifa za upotoshaji, zipuuzwe,” amesema Waziri Mkuu leo, Machi 24, 2020.

Machi 18, 2020 Waziri Mkuu aliagiza shule zote za awali, msingi na sekondari pamoja na vyuo kufungwa kwa kipindi cha siku 30, kama hatua za kuchukua tahadhari dhidi ya virusi vipya vya corona (Covid-19).

Aidha, aliagiza kusimamisha michezo yote ikiwemo ya ligi, kufunga maeneo ya kumbi za starehe; na kusitisha mikutano, semina, warsha inayoandaliwa na taasisi za umma na binafsi.

Serikali imeripoti visa 12 vya corona nchini huku mgonjwa wa kwanza kuripotiwa akibainika kuwa hana tena maambukizi ya virusi hivyo.

Rais John Magufuli amesema wageni wote wanaotoka nchi ambazo kuna visa vya virusi vya corona watalazimika kukaa karantini kwa siku 14 kwa gharama zao wenyewe. Rais aliagiza wale wote wanaotoa taarifa za uongo kuhusu ugonjwa huu wachukuliwe hatua haraka.

Serikali imeendelea kutahadharisha wananchi kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, na vyombo vya usafiri vya umma kuhakikisha havisimamishi abiria.

Mbowe athibitisha mwanaye kuugua corona, aeleza hali yake na alivyoupata
Fuata taratibu hizi wakati wa kunawa mikono