Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamisi Issah kuwasaka na kuwatia mbaroni watu waliohusika na wizi wa tani tano za nondo na kisha wakatoroka.

Ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wafanyakazi na wananchi mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa stendi ya mabasi ya kimataifa ya Moshi, katika kata ya Ngangamfumuni, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Amesema kuwa mradi huo ni maalum kwani uko miongoni mwa miradi ambayo Serikali imekuwa ikiweka utaratibu wa kupelekea fedha kwenye miradi iliyotengwa na Halmashauri.

“Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 9 za kuanzia mradi huu lakini inasikitisha kuona kwamba wanaMoshi mnahujumu kwa kuiba vifaa vya ujenzi. Ninazo taarifa kuwa hapa zimeibiwa tani tano za nondo na zimeshakamatwa.”

“Ni aibu, ni aibu kwa wana-Moshi. Ninyi wenyewe mnauhujumu huu mradi. Manispaa iweke utaratibu wa ulinzi ili vifaa vingine visipotee zaidi. Mkuu wa Wilaya chukua hatua ya kuwafuatilia wote waliohusika,”amesema Majaliwa.

Aidha, kupitia maswali aliyouliza, Waziri Mkuu alibaini kuwa walinzi wawili waliokuwepo siku ya tukio walitoroka ndipo akaamua kumwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa, awasake na kuhakikisha wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Ujenzi wa stendi hiyo kubwa unafanywa na mkandarasi mkuu ambayo ni kampuni ya CRJE ya China akishirikiana na wakandarasi wasaidizi watano na unatarajiwa kukamilika Januari 2021. hadi kukamilika, ujenzi huo unatarajiwa kugharimu sh. bilioni 28.8.

Ikikamilika, stendi hiyo ambayo itakuwa na ofisi, maduka, migahawa na hoteli, itakuwa na uwezo wa kuhudumia mabasi 300 kwa siku ambayo yataingia na kutoka. Kati ya hayo, mabasi 72 yanaweza kuegeshwa kwa wakati mmoja, pia kutakuwa na maegesho ya ya magari binafsi 218, teksi 34 na bajaji na bodaboda 20.

Wakati huohuo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamisi Issah amethibitisha kukamatwa kwa watu watano ambao wanatuhumiwa kuhusika na wizi wa tani tano za nondo katika eneo la ujenzi wa stendi hiyo lililopo Ngangamfumuni.

“Hawa watu tumewakamata jana jioni, na kati ya walinzi waliotoroka, tumemkamata mmoja wao tayari akiwemo mkazi wa Rau, Daudi Audifasi mwenye miaka 48 ambaye anadaiwa kutoboa ukuta wa uzio kwa chini, na kukutwa na nondo nyumbani kwake ambako ni mita 10 kutoka eneo la tukio.

 

 

Serikali kuanza kusajili nyaraka na hati miliki za ardhi ndani ya mkoa
Video: IGP Sirro atoa kauli polisi kuzuia mikutano ya wapinzani | 'Haponi mtu' CCM