Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amewahakikishia wananchi kuwa bei ya mifuko mbadala itaendelea kushuka.

Ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati akizungumzia tathmini ya kampeni ya katazo la mifuko ya plastiki lililoanza kutekelezwa na Serikali hapa nchini Juni mosi 2019.

Amesema kuwa hivi sasa viwanda vingi vinaendelea kuagiza mitambo ya kutengeneza mifuko mbadala na kuwa hadi kufikia Septemba mwaka huu bei itakuwa imeshuka na ubora wa mifuko hiyo utaongezeka.

Waziri Makamba amebainisha kuwa changamoto iliyojitokeza ni kwamba zuio la mifuko ya plastiki liliahirishwa mara kwa mara kwani lilishatangazwa siku za nyuma hivyo wawekezaji wa mifuko mbadala walidhani safari hii lingeahirishwa tena hivyo kupelekea kutoagiza mitambo ya kuzalisha mifuko mbadala kwa wakati.

“Hivi tunavyoongea tayari wenye viwanda na wafanyabishara wameshtuka na kuanza kutumia fursa hii kuingiza mitambo na kuzalisha kwa wingi mifuko mbadala,” amesema Makamba.

Akizungumzia kuhusu malalamiko ya ukubwa wa bei ya mifuko mbadala kutoka kwa wananchi amesema kuwa zamani ile mifuko ya plastiki si kweli ilikuwa inatolewa bure unaponunua bidhaa bali ilikuwa inajumuishwa na bei ya bidhaa yenyewe.

Aidha, ameongeza kuwa unapoleta mabadiliko ni lazima uzungumze na wadau na wananchi wayaone mabadiliko unayotaka kuleta kuwa yana manufaa kwao na hawawezi kuyapinga.

Hata hivyo, Waziri Makamba ameuhakikishia umma wa Watanzania kuwa mwenendo wa bei ya mifuko mbadala utaendelea kushuka kadri siku zinavyokwenda.

Inashauriwa kula karoti 6 kwa wiki, umuhimu wake watajwa hapa
Wenye viwanda watakiwa kuwa na Transfoma zao