Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Evodi Mmanda amepinga vikali tabia ya baadhi ya wazazi kuwafelisha kwa makusudi watoto wa shule za msingi kwa kuwaambia waandike majibu ya uongo kwenye mitihani yao wakiogopa kuwapeleka shule za sekondari.

Kupitia katazo hilo Mmanda ameagiza wazazi hao kukamatwa mara moja kwa tabia hiyo ya kuwafundisha watoto kujaza majibu ya uongo.

Agizo hilo limetolewa katika kikao cha wadau wa elimu ya halmashauri ya Wilaya ya Nanyamba, kufuatia shule ya msingi zaidi ya tano kubainika kuwa baadhi ya wazazi wamewafundisha watoto wao kujaza majibu ya uongo ili wafeli katika mitihani yao.

Kwa upande wa Maafisa Elimu wa msingi na sekondari katika Halmashauri ya Nanyamba, wamesema wamejipanga kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu shule na walimu ili wafanye vizuri kutokana na halmashauri hiyo kuwa nyuma sana kielimu.

Nao wadau wa elimu walioshiriki katika kikao hicho wametoa maoni yao juu ya suala hilo huku wakiitaka serikali kushughulikia kero hiyo pamoja na kuboresha miundombinu ya elimu katika halmashauri hiyo.

Video: "Nakufahamu wewe ni mpole, nakuomba ukaze kidogo sauti" - Mwakibolwa
Facebook wamfungia mwana harakati wa Ethiopia