Marekani imevunja rekodi baada ya kubaini zaidi ya watu 55,000 waliopata maambukizi ya virusi vya corona (covid-19) ndani ya siku moja, idadi ambayo ni kubwa zaidi kuwahi kuripotiwa duniani ndani ya siku moja tangu virusi hivyo vilipobainika.

Katika jimbo la Florida, juzi waliripoti visa vipya takribani 10,000 ndani ya kipindi cha saa 24. Texas, Arizona na California kwa pamoja wamerekodi karibu nusu ya idadi yote ya visa vipya vya corona.

Marekani ilirekodi visa 55,274 ndani ya saa 24, hali iliyosababisha kuipita Brazil iliyowahi kurekodi visa 54,771 ndani ya siku moja, Juni 19, 2020.

Rais Donald Trump amesema kuwa kuongezeka kwa idadi ya watu wanaogundulika kuwa na covid-19 kunatokana na kasi ya upimaji ambayo imeimarishwa kuliko nchi yoyote duniani. Lakini anaamini kuna habari njema kupitia taarifa hiyo kwakuwa idadi ya watu wanaopoteza maisha imeshuka.

“Kuna kupanda kwa kasi kwa visa vya corona kwa sababu upimaji wetu ni mkubwa na mzuri, zaidi na bora zaidi ya nchi nyingine yoyote. Hii ni habari njema, lakini habari njema zaidi ni kwamba idadi ya vifo IMESHUKA. Pia, vijana ambao wanapona haraka na kwa urahisi zaidi!” Trump ametweet.

Hadi leo, zaidi ya watu milioni 2.8 wameshabainika kuambukizwa virusi vya corona nchini humo, zaidi ya 857,000 wamepona na zaidi ya 131,000 wamepoteza maisha.

Real Madrid yajituliza kileleni

Nugaz: Sisi hatufungwi

Namungo FC watuma salamu Sahare, Tanga
Real Madrid yajituliza kileleni