Serikali imewaagiza watendaji wakuu na viongozi wote Serikalini kuzingatia kikamilifu mwongozo wa maandalizi ya mpango wa bajeti ya mwaka 2018/2019 ili uweze kuleta tija na kuendeleza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Agizo hilo limetolewa na Waziri Mkuu, mjini Dodoma, ambapo amewataka watendaji hao ambao ndio maafisa katika taasisi zao wahakikishe wanazingatia mambo yote muhimu yaliyoainishwa kwenye mwongozo ili kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa mpango wa bajeti.

Amesema kuwa miongoni mwa mambo ya kuzingatia ni ukusanyaji wa mapato ya ndani ambapo aliwataka maafisa masuuli kuhakikisha makusanyo yote yanawekwa kwenye mfuko mkuu wa Serikali.

“Maafisa masuuli waendelee kupunguza matumizi ya Serikali kwa kufanya tathmini ya uendeshaji wa taasisi zao ili kuchukua hatua stahiki na kuhakikisha taasisi zinazojiendesha kibiashara zinapata faida na kuacha kutegemea ruzuku kutoka Serikali kuu,” amesema Majaliwa.

Aidha,katika kudhibiti matumizi na kupunguza gharama, amewataka waendelee kufanya uhakiki wa watumishi ili mishahara ilipwe kwa watumishi wanaostahili na wanaopaswa kupandishwa madaraja wahakikiwe na malimbikizo yote ya madeni yabainishwe ili yaweze kulipwa.

Hata hivyo, ameongeza kuwa maafisa masuuli hao wanatakiwa kuhakikisha madai ya watoa huduma wote yanahakikiwa na mkaguzi mkuu wa ndani wa hesabu za Serikali na kuingizwa kwenye hesabu za fungu husika.

 

Dkt. Ndugulile alia na uhaba wa watumishi wa afya
Kiongozi wa dini kuongoza 'kikao cha jeshi' cha hatma ya Urais wa Mugabe