Watanzania 10,000 wanatarajiwa kunufaika na ajira katika mradi mkubwa wa bomba la mafuta ghafi la Afrika mashariki (EACOP) unaotarajia kuanza ujenzi wake mapema mwezi September mwaka huu ukiwa unapitia mikoa 8 wilaya 24 na kata 134 nchini Tanzania.

Hayo yamesemwa mkoani Kagera na Waziri wa Nishati, Medard Kalemani wakati wa kongamano la wadau wa Mkoa Kagera lililohusu mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki la EACOP.

Amesema kuwa katika ujenzi na utekelezaji wa mradi huo kipaumbele kitatolewa kwa Watanzania wa maeneo ambayo mradi huo unatarajiwa kupita kwa kuzingatia sifa na vigezo ambapo wananchi wa mkoa Kagera wanatarajiwa kunufaika zaidi kwasababu mradi huo unaanzia mkoani humo.

Waziri Kalemani amesema kuwa mradi huo utakuwa na kambi kubwa mbili katika mkoa wa Kagera ambazo zitakuwa katika wilaya za Misenyi na Muleba ambapo amewataka wananchi wamaeneo hayo kuchangamkia fursa zote zitakazotangazwa zikiwemo fursa za kusambaza vyakula, vifaa vya ujenzi, pamoja na fani mbalimbali.

“katika mkoa wa Kagera kata 20 zitapitiwa na mrdi huu, vijiji 34 na vitongoji 117, kwa hiyo wana Kagera watakuwa na wajibu mkubwa sio kulilinda tu lakini kupata fursa nyingine. tukumbuke ambapo bomba hili litapita miji itakuwa hivyo na ulinzi utaimalika zaidi.”amesema Kalemani

Kwa upande wake Naibu waziri wa nishati, Subira Mgalu ambaye ni mlezi wa mkoa wa Kagera kwa upande wa nishati amewataka wananchi wa Kagera kuchangamkia fursa hiyo na kuahidi kutoa ushirikiano ili kufikia faida za mradi huo kwa wana Kagera, na kuongeza kuwa vijiji vyote vitakavyopitiwa na mradi wa bomba la mafuta vitapelekewa umeme.

Naye Mkuu wa mkoa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti amemhakikishia waziri wa nishati kuwa wananchi wa Kagera wapo tayari kuupokea mradi huo mkubwa na fursa zote zitakazojitokeza wanakagera watazichangamkia.

Bomba hilo la mafuta ghafi la Africa Mashariki EACOP lenye urefu wa km 1445 litapita katika mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.

DC Kassinge aonya kuhusu mifuko ya rambo, ' tukikukamata utapata tabu sana'
Watu 12 wameuawa kwenye jumba la Serikali Marekani