Tanzania imejipanga kuwapokea na kuwatembeza watalii zaidi ya 1000 kutoka Israel wanaokuja nchini kutembelea vivutio mbalimbali mwezi Octoba 2019.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Faraji Mnyepe imesema kundi la kwanza lililokuwa na zaidi ya watalii 200 liliwasili nchini Oktoba 5, 2019 na kundi la pili lenye zaidi ya watalii 520 linatarajiwa kuwasili Oktoba 12, 2019.

Taarifa hiyo imesema kundi la tatu lenye watalii zaidi ya 200 litawasili nchini Oktoba 13, 2019 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa  wa Kilimanjaro (KIA), na kwamba Watalii wengine zaidi wanatarajiwa kuwasili nchini mwezi huu baada ya Makampuni ya Uwakala wa Utalii kukamilisha taratibu za safari.

“ujio wa watalii hao unatokana na jitihada za kuitangaza nchi zinazofanywa na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Israel kwa kushirikiana na wadau wa utalii  wa ndani na nje ya nchi,” imesema sehemu ya Taarifa hiyo.

Hata hivyo Taarifa hiyo imesema inawakaribisha watalii hao kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini na baada ya kujionea wakawe mabalozi wazuri wa kuitangaza Tanzania nchini kwao na kwingineko.

 Watalii hao wanatarajiwa kutembelea Visiwa vya Zanzibar, Hifadhi za Taifa za Serengeti, Tarangire na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Mahakama Kuu yatengua hukumu ya Sugu
Monalisa kuinua vipaji kwa watoto wa kike