Wimbi kubwa la wasomi waliopo mitaani kukosa ajira nchini limetajwa kusababishwa na vijana wengi kutozingatia kile wanachofundishwa vyuoni na badala yake kujikuta wakihitimu elimu ya juu bila kujua nini watakwenda kufanya wawapo uraiani.

Katika mahafali ya 16 ya chuo cha ufundi cha manamba mpechi kilichopo mjini Njombe mhadhiri wa vyuo vikuu nchini kwa ngazi ya udaktari dkt. Rechion Kimilike ambaye alikuwa mgeni wa heshima  amesema kuwa vijana takribani milioni kumi kila mwaka wanaingia katika soko la ajira lakini waliowengi  hawana stadi za maisha wala  stadi za kazi jambo linalosababisha  wengi wao  kukata tamaa pale wanapokosa ajira.

“Vijana wa sasa hivi ni wanyonge hawajiamini katika maisha yao na kukosa kujiamini kunawasukuma kuingia kushiriki katika mambo machafu na mambo ya fujo, wengine wameingia katika hali hatari zaidi na mbaya zaidi wengine wanakuwa ni wahanga na kuwa zana za vurugu za kidini au fujo za kisiasa, hivyo vijana wetu wanapokosa ajira ni tishio la utulivu wa kisiasa” amesema Kimilike

Mkuu wa chuo hicho bwana Daniel Ole M’bezi anasema mbali na kukabiliwa na changamoto mbalimbali lakini kimefanikiwa kupata uwakala  toka chuo cha usafirishaji taifa NIT kwa ajili ya kutoa mafunzo ya udereva ambao utamsaidia mwanachuo kupata ajira serikalini.

Joseph Lutumo,Charity  Julius na Mary  Makundi  ni wahitimu wa elimu ya ufundi katika chuo hicho wamekiri kuwa ujuzi waliojifunza kwa kipindi chote utakwenda kuondoa kabisa changamoto ya kutegemea ajira serikalini kwani wanaweza kuitumia elimu hiyo  kwa kubuni miradi mbalimbali.

Regina Lindi anawakilisha kundi la wazazi wa wanafunzi hao ambaye amesema hatarajii kuona vijana wao wanakwenda kujiingiza katika makundi  yanayokinzana na tabia njema huku wakitaka gharama walizozitumia kuwasomesha zirejeshwe kwa kwenda kuchapa kazi kwa bidii.

Jumla ya wahitimu 96 wa kozi mbalimbali wamefanikiwa kuhitimu masomo yao katika fani mbalimbali ikiwemo utalii katika chuo hicho.

ACT- Wazalendo yatoa masharti 7 kushiriki uchaguzi, ''Uanze upya"
Barua nzito, Aliyejinyonga Tarime "Msiwaamini Waganga fanyeni kazi halali"