Mkuu wa wilaya ya Ludewa mkoani Njombe Adrea Tsere ametangaza kumuweka lumande “Lock up” mwananchi yeyote atakayeshidwa kuwa na zao la biashara kutokana na uhamasishaji mkubwa unaoendelea wilayani humo ili kukuza uchumi wa wilaya na wananchi wa wilaya hiyo.

Mkuu wa wilaya hiyo amesema uamuzi huo katika kikao cha hamasa cha wadau/wanaLudewa wanaoishi nje ya wilaya kilichofanyika mjini Njombe, na kutokana na sheria ndogo walizojiwekea ili kuhakikisha kila mtu anakuwa na zao la biashara kwa kuwa wilaya hiyo imekuwa ikikubali mazao mbali mbali ya kibiashara likiwemo zao la korosho, chai na kahawa hivyo sheria kali zitachukuliwa kwa mwananchi ambaye hataweza kushiriki katika mazao hayo.

“Akiwa Lock up tutakuwa tunamuelimisha umuhimu wa kupanda korosho, akielewa akiahidi kwamba atapanda tutamuachia aende kupanda korosho,lakini kwasababu tumetunga sheria kama ataendelea kuwa mkaidi tutampeleka mahakama ya mwanzo kwasababu kuto kupanda zao la biashara ni ukiukwaji kwa mujibu wa sheria ndogo ya halmashauri na kama watakuwa wengi tutawachukuwa kwa viwango”anasema Adrea Tsere

Amesema mkuu wa wilaya amepewa mamlaka na Rais kwa mujibu wa sheria ya kumuweka mtu yeyote masaa 24 hakutakuwa na swali lolote ni lazima mkaidi apelekwe Lumande kwakuwa ajenda iliyopo kwa sasa ni kujenga uchumi huku mazao hayo yakiwa ni mali yao wananchi

Katika hatua nyingine, ameongeza kuwa ili kuimarisha ufaulu wa elimu ya sekondari wilayani Ludewa, wananchi na watumishi wa wilaya hiyo wameanza kuchangia shilingi milioni 41 na tayari zipo katika mfuko wa elimu kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari ya vipaji maalumu kwa kuwa licha ya baadhi ya wanafunzi kupata ufaulu mzuri lakini wilaya hiyo imekosa shule ya vipaji.

James Mwinuka,Edgar Mtitu na Padre Lugome ni baadhi ya wakazi wa wilaya ya Ludewa wanaoishi Njombe mjini wamekiri kulipokea wazo hilo kwa mikono miwili na kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa serikali ya wilaya yao.

Kwa takribani miaka minne  mfululizo halmashauri ya wilaya ya Ludewa imekuwa ya mwisho kitaaluma kati ya halmashauri sita za mkoa wa Njombe hatua ambayo imefanyiwa kazi na mkuu huyo wa wilaya kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi wa ludewa.

Video: Hakuna wanawake wanaojifungulia chini Muhimbili
Mahiga aitaka THBUB kuimarisha utawala bora