Wakati tunaelekea katika uchaguzi mkuu, Oktoba 25 mwaka huu, tumekuwa tukishuhudia mambo mengi yanayoendelea na propaganda na mvutano hasa kati ya timu ya wagombea wawili wa nafasi ya Urais, Edward Lowassa (Chadema) na Dk. John Magufuli (CCM).

Joto hili la uchaguzi mkuu linaloonekana kuwa kali zaidi katika historia uchaguzi wa vyama vingi nchini, limetengeneza timu mbili kubwa katika kila tasnia na hata taasisi mbalimbali nchini.

Moja kati ya changamoto kubwa iliyoonekana na kuzua zogo mitandaoni, ni uamuzi wa baadhi ya wasanii wakubwa nchini kujiingiza katika siasa na kuwapigia debe waziwazi wagombea urais, hali iliyozua sintofahamu kwa mashabiki wao ambao wana itikadi tofauti za vyama.

Kati ya wasanii ambao wamejitokeza kumuunga mkono Mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli ni pamoja na Diamond, Mwana Fa, Wema Sepetu, Steve Nyerere na wengine. Na wale waliojitokeza kumuunga mkono wazi Edward Lowassa ni pamoja na Nikki Mbishi, Jackline Wolper, Aunt Ezekiel na wengine.

Baadhi ya mashabiki wao ambao wanaonekana kuwa na itikadi tofauti wamekuwa wakiwashambulia kwa lugha kali, wengine wakitangaza kuwa- unfollow kwenye mitandao hiyo huku wengine wakidai kuwa wamesahau misingi baada ya kupewa fedha na wagombea wanaowasapoti.

Ni dhahiri kuwa wasanii hawa wakubwa wana ushawishi mkubwa katika jamii na ndio sababu wana siasa wamewaona kama sehemu ya kete yao muhimu ya kuwapeleka Ikulu.

Hapa tunawaweka pembeni ya mjadala wasanii ambao wamejitokeza kujiunga na vyama na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa kisiasa.

Je, wanapatia au wanakosea?

Tukianza kuangalia uzoefu wa mataifa yaliyoendelea kidemokrasia kama Marekani, tunakumbuka kuwa wasanii wengi walijitokeza kumpigia debe rais Barack Obama kabla ya kuingia madarakani na wakati anaomba ridhaa ya kuendelea na awamu ya pili.

Jay Z ambaye ndiye aliyekuwa akiongoza kampeni akiwahimiza vijana kumchagua rafiki yake Barack Obama. Alifikia hatua ya kuubadili wimbo wake maarufu ’99 Problems’ kuwa wimbo unaomsapoti Obama na kumponda mpinzani wake.

Jay Z alifanya hivyo akifahamu kuwa mashabiki wake wana itikadi tofauti tofauti na wengine walimponda kwa upande aliouchagua lakini alicheza kete nzuri sana kumfanya Obama aungwe mkono na vijana wengi kwenye uchaguzi wa awamu ya pili ya Obama ambao ulionekana dhahiri kuwa mgumu kwake.

Ilifikia hatua watu walifanya mzaha na kumlaumu Jay Z pale Barack Obama aliposhindwa kwenye mdaharo wa kwanza dhidi ya wapinzani wake. Utani wa kwenye mitandao ya kijamii ulidai kuwa ‘huenda Obama alimsikiliza zaidi Jay Z kuliko washauri wake wa masuala ya kisiasa’ ndio sababu alishindwa kwenye mdaharo huo.’ Hata hivyo alishinda kwa kishindo katika midaharo iliyofuata.

Hivyo, kwa kiasi kikubwa ushawishi wa wasanii wakubwa nchini wana nafasi yao katika kuwaongezea kura wagombea urais. Kwa hiyo, nguvu yao isipuuzwe hata kidogo, au kwa Kiswahili kisicho rasmi ‘isichukuliwe poa’.

Hebu fikiria, kuna watu wangapi ambao wanavaa kama msanii fulani, wanaongea kama msanii fulani na hata wakitamani kuwa yeye siku moja? Kwa weledi wa masuala ya uandishi tunaikumbuka vizuri ‘culturalisation theory’ katika hili. Watu hao wana nafasi kubwa sana ya kubadilisha uamuzi wao pale msanii huyo anapowashawishi. Na ni wengi katika jamii ya Tanzania hasa wale wa matabaka ya chini.

Hata hivyo, ingawa wasanii wanaowapigia kampeni wagombea wanafanya hivyo kwa kufurahia haki ya na uhuru wao kikatiba, kuna dalili kubwa kuwa wengi wanauchukulia uchaguzi mkuu huu kama fursa ya kibiashara na kutengeneza pesa nyingi kwa kuwasapoti wagombea fulani.

Katika hatu nyingine, ipo hasara ambayo inaonekana dhahiri kuwa itawatafuna wasanii hawa kwa Tanzania kwa kuwa ingawa tunayo demokrasia, bado sehemu kubwa ya watanzania hawana elimu ya uraia kama wale wa nchi zilizoendelea ikiwamo Marekani tuliyoitolea mfano.

Wapo ambapo kutokana na hasira zao dhidi ya mgombea fulani, wanapoona msanii waliyekuwa wanampenda akimsapoti mgombea huyo huanza kumchukia ghafla na kumuona hafai au hana upeo wa kutosha kama walivyodhani awali. Ukisoma comments kwenye posts za wasanii wanaoweka picha za wagombea au logo zao utaona hili.

Bado kuna hasara kubwa ya kutengeneza matabaka kati ya mashabiki ambao wanambeba msanii na kumfanya awe alivyo. Hasara hii ni kubwa na inaweza kuonekana kwa wakati huu kama haina maana lakini wakati mwingine inaweza hata kumnyima msanii fulani ushawishi hasa pale anapotakiwa kujiunga na kampeni nyingine zisizokuwa na itikadi ya siasa. Mashabiki walewale wanaweza kumuona kama ‘hafai kuwakilisha kile anachokisema’. Silaha kubwa hapa ni kuwa ‘nutral’ na kufanya muziki wako tu, au uwahamasishe watu kupiga kura bila kuwaelekeza nani wampigie, hiyo ni kazi bora zaidi na tumeona baadhi ya wasanii wakifanya hivyo, na tumesikia nyimbo zao pia.

Lakini, mwanafalsafa mmoja aliwahi kusema kuwa matatizo na changamoto duniani ni sehemu ya maisha ya binadamu, na kama unataka kuyaepuka unatakiwa kuwa nje ya dunia kisaikolojia.

Ili msanii asiingie kwenye dhoruba ya kuwagawa mashabiki wake na kuchukuliwa katika mlengo fulani, ni vyema zaidi akajiweka pembeni ya kampeni. Lakini kama amepima atakachopata na atakachokosa kwa mashabiki wake, uamuzi aliochukua utabaki kuwa ndio uamuzi sahihi zaidi kwake. Uamuzi huo unapaswa kuheshimiwa na watu wote ili mradi tu hauvunji sheria na hauingilii uhuru wa mtu yeyote.

 

Kuhusu Mgombea Ubunge Wa Chadema Aliyevamiwa...
Lowassa Amtegea Magufuli