Wanawake wanaojifungulia nyumbani badala ya hospitalini katika Wilaya ya Kibondo Mkoani Kigoma, hupigwa faini wanapoenda hospitalini kwa ajili ya kupata huduma endelevu za uzazi.

Hayo yamebainika kupitia ziara ya Mbunge wa Muhambwe, Mhandisi Atashasta Nditiye (CCM) ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, aliyezuru eneo hilo jana.

“Wake zetu wanapigwa faini ya kati ya Sh.20,000 na Sh.50,000 wanapoenda kupata huduma kwenye zahanati zetu baada ya kujifungulia nyumbani,” alisema Nicolaus Sabuni, mkaazi wa eneo hilo.

Kauli yake iliungwa mkono na baadhi ya wananchi waliokuwa katika ziara hiyo, ambao walimuomba Mhandisi Nditiye kuchukua hatua kukomesha hali hiyo.

Akijibu madai hayo, Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Innocent Sunamie, alikiri kuwepo kwa tabia hiyo na kwamba wameshawapiga marufuku wauguzi na watendaji waliokuwa wanawalipisha akina mama faini hizo.

“Tutafuatilia kwa karibu sana kuona kama tabia hizi bado zinaendelea na tutawachukulia hatua kali watakaobainika kuendeleza tabia hizi,” alisema Sunamie.

Naye Mhandisi Nditiye alionya vitendo hivyo na kueleza kuwa Serikali haitavumilia kuona baadhi ya watumishi wanafanya vitendo ambavyo vitasababisha mgogoro kati ya Serikali na wananchi wake. Aliagiza tabia hiyo ifuatiliwe na kukomeshwa mara moja.

LIVE: Yanayojiri Bungeni Dodoma leo Mei 21, 2019
Wanafunzi wanaofanya vibaya darasani kuwatia hatiani wazazi wao Njombe