Imeandikwa na Enosh Gabriel; Mhitimu Shahada ya Sheria, SAUT

Katika jamii zetu kumekuwa na misemo mbalimbali inayotumika ili kuonya juu ya baadhi ya mienendo na tabia ambazo wakati mwingine zinaweza kuwa si kosa kisheria lakini ni kinyume na maadili na utamaduni wa jamii husika.

Misemo hii imeweza kujenga tabia na kuzaa matunda kutoka katika ngazi za chini kabisa katika jamii hadi ngazi za juu kitaifa. Lakini kuna dalili za kutotumika tena kwa misemo hii katika jamii zetu kutokana na tabia ya kuziboresha zaidi na kupindisha maana na malengo yake halisi.Mfano ‘samaki mmoja akioza, unamtoa na kumtupa’.

Hebu tuvute kumbukumbu kidogo za matukio kadhaa, machache yaliyoonekana kusahaulika kiurahisi kwa kuwa hakuna aliyeweza kumfunga paka kengele. Na huenda aliyefungwa kengele hakuwa paka mhusika.
Tukumbuke majibu ya kada mkongwe wa CCM, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru katika mkutano wake na waandishi wa habari alioufanya kwa lengo la kuelezea kutoridhishwa na mwenendo wa chama chake katika mchakato wa kumpata mgombea wa Urais wa CCM, baada ya jina la Edward Lowasa kukatwa ‘kibabe’ katika kinyang’anyiro hicho.

Baada ya kuulizwa swali kwanini wakati wa Richmond alikuwa mbunge lakini hakuonekana kumtetea Lowasa ila amejitokeza leo? Mzee Kingunge alitoa majibu ambayo kwa maoni yangu yalilenga kuficha siri kama ilivyokuwa. “Niliona mambo yameharibika,nikakaa na Lowasa nikamshauri awajibike kisiasa.” Asante kwa jibu lake, lakini bado linaongeza swali kama uliona mambo yameharibika, Je, nani aliyeyaharibu mambo? Nani alipaswa kuvishwa kengele?
Kingunge

Majibu kama haya yanaashiria kuwa fedha za umma zinazopotea kutokana na ubadhilifu wa watawala zinaonekana kutowahusu wananchi hivyo kupoteza sifa ya kujua ukweli juu ya jambo lolote kuhusu upotevu wake.
Jambo hili linakiuka misingi ya katiba ya Jamhuri ya Muungano inayotaja uwepo na Uwajibikaji na Uwazi (Accountability and Transparency) wa Serikali juu ya mambo yanayowaathiri walipa kodi wake amabacho ni chanzo cha mapato yake.

Kwa kauli hizi mbalimbali za watu wanaoaminika kuwa karibu zaidi na watawala yanatia shaka juu ya mtu sahihi anaepaswa kulengwa na tuhuma hizo nzito zilizoshindwa kufikia mwisho kwa kuweka wazi mrejesho wake kwa jamii.

Hali hii inapelekea uwepo wa imani kwa baadhi ya watu kuwa inawezekana kuna watu nyuma ya pazia wasioruhusiwa kuguswa kwa namna yoyote ile juu ya madhambi wanayoyatenda. Au labda waliotenda wanasingizia uwepo kivuli cha wakuu wao wa kazi ili hali wanajua wao ndio chanzo. Yote yanaweza kuwa majibu sahihi.

Kwa bahati mbaya watuhumiwa wanajitetea tu kuwa hawakuhusika huku machoni pao wakionekana kuwanyooshea vidole wengine.

Nani muhusika mkuu wa “masakata” haya? EPA,ESCROW,RICHMOND,DOWANS na mengine mengi. Nani wa kulaumiwa? Je, ni yule anaedaiwa kuwa alificha siri kwa kujitolea kuumia kwa niaba ya wengine? Au mkubwa anaedaiwa kuwa anaujua ukweli wote ila kwa makusudi aliamua kumbebesha mzigo?

Bila shaka wote wanapaswa kubeba mzigo huu bila malalamiko kwa kutoweka wazi wahusika sahihi. Kuna msemo unasema SAMAKI MMOJA AKIOZA WOTE WAMEOZA. Baba wa taifa hili liliojipatia sifa ya kuwa kisiwa cha amani, Hayati Mwl. J.K.Nyerere aliwahi kusema katika moja ya wosia wake kwa taifa hili kuwa mpokeaji na mtoaji rushwa ‘WOTE MANZI GA NYANZA.’ Msemo wa lugha ya Kizanaki unaomaanisha wote ni walewale (maji ya ziwa).

Kauli hii inabeba maana nyingi kulingana na muktadha husika huku maana yake kuu ikiwa kwamba, anaetenda kosa na anaesababisha kosa kutendeka wote wawili wanawajibu sawa mbele ya sheria. Katika nyanja ya sheria juu ya makosa ya jinai mtu aliesaidia kosa kutendeka kwa namna yoyote ile anawajibika kisheria(Acsessories).

Kwa bahati nzuri mamlaka ya kuwawajibisha watawala wakuu wa nchi yako mikononi mwa wananchi kupitia wawakilishi wao bungeni kwa kupigiwa kura ya kutokua na imani nao(Vote of no Confidence for the Prime Minister & Impeachment for President).

Njia nyingine ni kupitia kura katika uchaguzi mkuu kwa kuindoa serikali iliyopo madarakani kupitia wingi wa kura kwa kuchagua chama kingine cha siasa, ingawa fursa hii hupatikana mara moja tu kila baada ya miaka mitano hapa nchini. Misemo kama hii ya ‘Samaki’ na ‘Manzi ga Nyanza’ ina faida na hasara zake.

Lakini katika nyanja ya kisiasa katika utawala ulioghubikwa na Usiri mkubwa juu ya mienendo yake mibovu katika uongozi unapaswa kutumika kama ulivyo, kwa lugha ya kisheria hujulikana (mutatis mutandiz).

Kutokana na makosa kama haya yanayojirudia mara kwa mara katika taifa letu, ni wajibu wetu wananchi kuchukua hatua stahiki pale tunapopata fursa ya kuwachagua wale watakaobeba dhamana kubwa ya taifa letu.

Hata hivyo, upande wa pili wa wapinzani nao bado kuna matatizo japo hawajapewa hata nusu ya nchi kuiendesha. Natambua kuwa hakuna mkamilifu, lakini sio ukamilifu wa imani, tunataka watu watakaosimamia katiba na kufanya maamuzi sahihi.

Mwalimu wangu wa SAUT aliwahi kunambia kuwa unapofanya makosa hutakiwi kusema ‘mbona fulani…’ wa ngazi za juu amefanya kwa kuwa “Dhambi itabaki kuwa Dhambi tu hata akiifanya Malaika wa Mungu haitabadilika.”

Leo sitawagusia sana walio nje ya uwanja wa mfumo wa madaraka yaani wapinzani ambao pia wana yao ambayo yanaonesha kuwa meli yao ina matundu madogo ambayo wasipoyaziba, itakuwa vigumu kuwavusha watanzania kwenye bahari ya Umasikini, Ujinga na Madhadhi.

Ni kura pekee ndio silaha tuliyonayo itakayotoa majibu ya malalamiko yetu na maumivu yetu kwa vitendo.

Misululu na matukio ya watanzania kudamka usiku wa manane kwa ajili ya kuandikishwa kwenye mfumo wa upigaji kura wa BVR unaweza kutoa matumaini kuwa huenda watanzania wameamua kweli kupiga kura mwaka huu na kumchagua wamtakae.

Hata hivyo, napata wasisi kama misululu hiyo ina uhusiano wa dhati na upigaji kura. Naamini wapo watanzania wengi ambao wanatafuta kitambulisho hicho kwa ajili ya kuwasaidia katika masual mengine pale wanapohitajika kutambulika.

Utambulisho wako hautakuwa na maana sana kama hautautumia vyema kuchagua aina ya utawala unaoutaka. Ukishindwa kuchagua watawala wa mfumo wa maisha yako, umechagua kushindwa katika mfumo wa maisha yako.

Tusipake rangi matatizo kwa kuyaita changamoto, tufanye kweli Oktoba kwenye sanduku la kura. Kama unaamini tatizo ni mfumo, fanya mabadiliko kwa vitendo kwa kuwa wote ‘Manzi ga nyanza’.
Imeandikwa na Enosh Gabriel Muhitimu Sheria Chuo kikuu Cha Mt.Augustine (SAUT)

Wojciech Szczesny Aliachia Goli La Arsenal
NATO Yaitisha Kikao Cha Dharura Kujadili ‘Mchezo Wa Vita’