Wananchi  wanaoishi eneo la shule ya Sekondari St Anney Trust (kipagamo) mjini makambako mkoani Njombe, wametishia kugoma kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 24 mwaka huu baada ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Makambako  Paulo Malala kuwataka wananchi hao kushiriki uchaguzi katika mtaa wa Magongo  badala ya mtaa wa Kipagamo kama ilivyo kuwa awali.

Wananchi wamesema wanashangazwa na kitendo cha mkurugenzi kuwaambia wanatakiwa washiriki uchaguzi wa serikali za mitaa katika mtaa wa Magongo badala ya mtaa wa Kipagamo ambao miaka yote wamekuwa wakihudumiwa na serikali ya mtaa huo.

“Mimi ninajitambua ni mkazi wa Kipagamo ninaambiwa leo niende Magongo, Magongo hakuna shule, kanisani naenda Kipagamo hata ugali ninaokula leo na wanangu nalima Kipagamo leo naambiwa niende Magongo nisikokujua, mimi siendi na kama ni kupiga kura ni bora nisipige kura, tunaomba mhe. Rais atusikie tunachotendewa watu wa Kipagamo” alisema mmoja wa wananchi kwenye mkutano

Awali akizungumza na wananchi katika eneo hilo ambalo lina mgogoro wa kimpaka kati ya serikali ya mtaa wa Kipagamo na mtaa wa Magongo mkurugenzi amesema, wananchi hao wanaoshi katika eneo hilo la shule hiyo ya sekondari wanatakiwa kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura na kushiriki uchaguzi katika mtaa wa Magongo badala ya mtaa wa Kipagamo.

“Kwa mujibu wa uchaguzi huu mpaka ni hili bonde ukitoka hapa kwenda kujiandikisha Kipagamo kutoka kwenye eneo hili utakuwa unavuruga uchaguzi, tutajadiliana mpaka kesho lakini maelekezo kwa ajili ya uchaguzi huu ndio hayo hatuwezi kuacha kuwaambia ukweli ulivyo”alisema Malala

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Magongo Alois Nyaulingo na mwenyekiti wa mtaa wa Kipagamo Keneth Kibiki kila mmoja amevutia upande wake kwamba eneo hilo ni la kwake.

“Nilivyokuwa napokea mtaa huu sikuonyeswa mpaka huu mheshimiwa mkurugenzi,lakini wazee waasisi walinionyesha eneo hili kuwa mwisho ni bonde la st.Anney”alisema Alois Nyaulingo mwenyekiti wa Magongo

“Na mimi nasumbuka lakini sisi tulisema hebu tutulie wananchi mpaka waje wataalamu watuonyeshe vizuri mwisho wa mtaa wetu”alisema Keneth Kibiki mwenyekiti wa Kipagamo

Diwani wa kata ya makambako Daud Tweve na diwani wa viti maalumu Pepetua Ngongi wamewataka wananchi hao wakubaliane na mkurugenzi ili waweze kushiriki uchaguzi huo na baada ya uchaguzi kuisha mgogoro huo wa kimipaka utafanyiwa kazi.

Mgogoro wa kimipaka kati ya serikali ya mtaa wa Magongo na serikali ya mtaa wa Kipagamo una mwaka mmoja tangu uibuke na mpaka sasa haujapatiwa ufumbuzi.

Video: Lupita Nyong'o asimulia alivyonyanyapaliwa kwa weusi wake
RC Makonda azindua utaratibu wa kupokea kero, malalamiko ya wananchi Dar