Wananchi wa Kijiji cha Nkwimbili Kata ya Lupingu Mwambao wa Ziwa Nyasa wilayani Ludewa mkoa wa Njombe, kwakutumia zana za mikono wameanza Rasmi uchimbaji wa Barabara ya kutoka Kijijini hapo itakayo waunganisha na Kijiji cha Nsisi Kata ya Lifuma, katika ukanda huo wa Ziwa Nyasa.

Wananchi hao wamesema kuwa wameamua kuunganisha nguvu zao na kuanza uchimbaji huo ili Serikali na Wadau wengine akiwemo Mbunge wa Jimbo hilo waone juhudi hizo na kutafuta njia bora ya kuwaunga mkono.

“Sisi Wananchi tumekubaliana pamoja kuanza kuchimba Barabara hii ambayo ni muhimu sana kwa maendeleo yetu, pia lengo letu tunataka Serikali ione hiki tunachokifanya hatimaye iweze kutuunga mkono kwa kutusaidia angalau mashine ya kuchimba Barabara hii kwa ubora zaidi,” Wamesema baadhi ya Wananchi.

Aidha, katika kuwaunga mkono Wananchi hao kwa hatua za awali, Mbunge wa Jimbo la Ludewa, Deo Ngalawa amewakabidhi vifaa vya kufanyia kazi yakiwemo Majembe, Chepe, Sululu na Mitalimbo pamoja na kuchangia mbuzi na Ng’ombe mmoja kwaajili ya mboga ya Wananchi wakati wa kazi.

Mbunge huyo ameahidi kuendeleza ushirikiano kwa Wananchi hao ikiwemo kuishauri Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kuhakikisha inazitambua na kuzichukua Barabara mbalimbali zilizoanzishwa kwa nguvu za Wananchi Wilayani Ludewa ili ziweze kuendelezwa kwa ubora unaostahili.

Faida 6 za kula pilipili mwilini
Habari Picha: Rais Magufuli alipowasili katika uapisho wa Ramaphosa Afrika Kusini