Wananchi wa Kijiji cha Mtulingala Kata ya Kitandililo Halmashauri ya mji wa Makambako mkoani Njombe kwa kushirikiana na Serikali pamoja na viongozi wao wameamua kujenga Zahanati Kijijini hapo ili kupunguza changamoto ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya Afya.
 
Wakizungumza na Viongozi wa chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Njombe waliofika kijijini hapo, wananchi wa Mtulingala wamesema kuwa wanalazimika kutembea umbali wa zaidi ya Kilomita tano kutoka kijijini hapo hadi Makambako mjini ili kufuata matibabu pindi wanapougua.
 
“Tumeamua kujenga Zahanati hapa kijijini baada ya kuona tunatembea umbali mrefu sana kufuata huduma za Afya, pia tunaishukuru Serikali kupitia viongozi wetu akiwemo Mbunge mh. Deo Sanga (Jah People) ameweza kutuchangia Bati zakutosha kwaajili ya kupiga paa jengo hili,” wamesema Wananchi wa Mtulingala.
 
Kwa upande wake, diwani wa Kata ya Kitandililo, Imani Fute ameeleza kuwa Jengo la Zahanati hiyo limejengwa kwa ushirikiano mkubwa kati ya Wananchi na Viongozi wa kata hiyo pamoja na Mbunge ambao wameshiriki kutoa michango mbalimbali iliyowezesha jengo hilo kufikia hatua ya ukamilishaji.
 
Amesema wananchi wa Kijiji hicho waliamua kujitoa na kuonesha umoja na ushirikiano katika ujenzi wa Zahanati hiyo kutokana na tatizo wanalokutana nalo la kutembea umbali mrefu kwenda kufuata huduma za Afya, hivyo kukamilika kwa Zahanati yao kutawezesha kumalizika kwa tatizo hilo.
 
Hata hivyo, Chama cha Mapinduzi CCM mkoa wa Njombe kupitia kwa Katibu wake wa siasa na uenezi mkoani humo, Erasto Ngole kimepongeza juhudi hizo za wananchi za kuunga mkono chama na Serikali huku akikabidhi pesa kiasi cha Tsh, 200,000/= mchango wake katika kuunga mkono juhudi za wananchi.

Maelfu ya wananchi waandamana Morocco
Bobi Wine kufanya maandamano Uganda