Baadhi ya wanajeshi wa vikosi vya jeshi la Nigeria, jana walifanya mgomo na kufyatua risasi juu wakiwa kwenye uwanja wa ndege wa jiji la Maiduguri, wakipinga kupelekwa tena kupambana na wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram bila kuzingatia haki zao.

Vyombo vya habari jijini humo vilieleza kuwa wanajeshi hao waligoma kupanda ndege iliyokuwa inatakiwa kuwatoa Maiduguri na kuwapeleka katika mji wa Marte ulioko Borno karibu na mpaka wa nchi hiyo na Niger.

Mashuhuda wa mgomo huo walidai kuwa wanajeshi hao walifyatua risasi juu kuanzia saa kumi na mbili na nusu jioni kwa takribani saa nne.

“Tumekasirika na ndio sababu tunafyatua risasi. Kwanini wanatupeleka kwenye eneo lingine kupambana baada ya kukaa miaka minne porini?” amesema mwanajeshi mmoja na kukaririwa na BBC.

Alidai kuwa awali waliambiwa watapigana vita hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu tu lakini wametumia miaka minne na sasa wanataka kuhamishiwa eneo lingine.

Msemaji wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege wa Nigeria, Henrietta Yakubu alisema kuwa mgomo ulimalizika na kwamba hali ya utulivu ilirejea. Alisema mgomo huo haukusabisha kufungwa kwa uwanja huo wa ndege.

Nigeria imeendesha oparesheni ya kijeshi dhidi ya wanamgambo wa Boko Haram kwa miaka tisa sasa. Serikali imekuwa ikieleza kuwa tangu mwaka 2015 imelishinda kundi hilo kiufundi.

DC Mjema aukataa mradi wa Maji
Samsung kuzindua 'memory Card' ya 512 GB