Walimu wilayani Kahama wamegomea maagizo yaliyotolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kuwataka kununua sare kwa ajili ya kuupokea Mwenge wa Uhuru ama kukatwa mishahara yao kulipia sare hizo.

Mwenyekiti wa Walimu Tanzania (TTU) wilaya ya Kahama, Victor Tandise amesema kuwa walipokea barua kutoka kwa Mkurugenzi wa Wilaya hiyo ikiwataka walimu wote kuhakikisha wanafika katika duka fulani kununua sare kwa shilingi 30,000 kwa ajili ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru Mkoani Shinyanga vinginevyo watakatwa kiasi hicho kwenye mishahara yao.

Akizungumzia sakata hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Deogratias Kapami alikiri kutoa maagizo hayo akisema kuwa ni lazima kwa mtumishi wa umma kushiriki katika shughuli za Mwenge wa Uhuru.

Kwa mujibu wa The Citizen, Alisema kuwa uamuzi wa kuwakata mishahara ulikuwa na lengo zuri la kuwasaidia walimu ambao hawana pesa kwa wakati huo na kwamba wangekatwa shilingi 30,000 kwa awamu mbili kwenye mishahara yao (15,000 kila awamu) kama gharama za sare hizo zinazoshoneshwa kwa vitenge).

“Kama kuna mtumishi wa umma ambaye sio raia wa nchi hii ambaye amejiingiza kinyamela nchini huku akijua sio Mtanzania, muache apinge kushiriki shughuli za mwenge wa uhuru. Lakini kama ni watumishi wa umma walio Watanzania halisi, lazima washiriki na wahudhurie wakiwa ndani ya sare maalum,” Kapami anakaririwa.

Alisisitiza kuwa baada ya Mwenge wa Uhuru kuondoka Mkoani humo, hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya walimu wote watakaokaidi agizo hilo.

Mwenge wa Uhuru unatarajia kuwasili Mkoani Shinyanga mwanzoni mwa mwezi Oktoba.

 

Audio: Lowassa - Magufuli anafanya vizuri, Asema CCM inafanya vizuri zaidi vjijijni kuliko Upinzani
Video: Hotuba ya Trump yakatishwa Kanisani, Mchungaji amgeuka