Wakulima wa Kilimo cha Umwagiliaji nchini kupitia Skimu za Umwagiliaji, wametakiwa kuwa na usimamizi thabiti wa skimu hizo ili kilimo hicho kiwe cha uhakika zaidi na chenye tija kwa mkulima na taifa kwa ujumla.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya KIlimo Mhandisi Mathew Mtigumwe, Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo na Utafiti, Wilhelm Mafuru amesema kuwa, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeendelea kusaidia wakulima kupata elimu kupitia wataalamu ili kuweza kulima kwa tija na kuendelea kusimamia kuimarisha shughuli za kilimo cha umwagiliaji.

Ameyasema jijini Dodoma kwenye kongamano lililoshirikisha vyama 36 na kushindanisha vyama vya umwagliaji 8 kutoka Kanda 8 za Umwagiliaji lenye lengo la kutoa motisha kwa skimu zilizowahi kupata mafunzo ya Matunzo na Uendeshaji chini ya Mradi wa kujenga uwezo kwa wataalamu wa Umwagiliaji wa TANCAID awamu wa pili kupitia Shirika la kimataifa la maendeleo la Japan JICA kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mbogo Futakamba amesema kuwa kuelekea Tanzania ya Viwanda kilimo cha umwagiliji kinahitaji uwekezaji mkubwa na miundombinu bora na mfumo sahihi wa umwagiliaji jambo ambalo linaweza kuleta uhakika wa chakula malighafi za viwanda na kilimo kuboreka kupitia mifumo sahihi ya umwagiliaji.

Aidha, warsha hiyo imetoa fursa kwa wadau wa umwagiliaji kuona namna ya kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji, pamoja na kutoa nafasi kwa vyama vya umwagiliaji kubadilishana uzoefu wa namna bora ya kuendesha na kutunza skimu za umwagiliaji.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima wa Skimu ya umwagiliaji ya Lemkuna, Frida Tarimo amesema kuwa kupitia mafunzo wanayopata wakulima wameweza kusimamia Uendeshaji na Matunzo ya miundombinu ya umwagiliaji, upatikanaji wa maji ya kutosha kwa vitalu na maandalizi mazuri ya kalenda ya msimu wa kilimo jambo ambalo ameeleza limeongeza uzalishaji katika kilimo hususani cha zao la Mpunga.

 

Serikali yawashika mkono wabunifu, yatoa milioni 700
Jenerali Kasike aanza ziara ya kikazi mkoani Kagera