Wakulima kutoka zaidi ya Skimu 100 za umwagiliaji nchini wamenufaika na mafunzo ya kukuza na kuboresha kilimo cha umwagiliaji hivyo kuongeza uzalishaji zaidi.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa mkutano wa Tano wa Kamati ya Pamoja ya Uratibu wa Mradi wa kujenga uwezo kwa wakulima wadogo wadogo Awamu ya pili (TANCAID II) Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Marco Ndonde amesema kuwa wakulima walionufaika na mafunzo hayo wanatoka kwenye Kanda zote nane za Umwagiliaji nchini.

Amesema kuwa mradi wa TANCAID II uliofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) tangu mwaka 2015 umejikita katika kujenga uwezo wa wakulima wadogo wadogo ambao ulitekelezwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) ukiwa na lengo la kukuza na kuboresha sekta ya umwagiliaji nchini.

“Baada ya mafunzo haya Wakulima katika Skimu mbalimbali nchini sasa wanauwezo wa kuibua miradi inayowaletea faida na kuitekeleza kwa ufanisi na hivyo kuongeza uzalishaji wa mazao yao,”amesema Ndonde.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa mradi wa TANCAID II, Anthony Nyarubamba amesema kuwa chini ya mradi huo NIRC imetumia wataalamu wake kuandaa miongozo kabambe ya umwagiliaji (CGL) ambayo imeanza kutumika na wakulima katika maeneo mbalimbali hususani katika Skimu za umwagiliaji.

Aidha, amesema kuwa wakulima sasa wanaweza kusimamia skimu zao za umwagiliaji katika ngazi mbalimbali kuanzia uibuaji wa miradi hadi usimamizi wa miundombinu inayojengwa na serikali badala ya kuiacha iharibike kama ilivyokuwa awali.

Nyarubamba ameongeza kuwa miongozo kabambe imewajengea wakulima uwezo wa kutunza taarifa ya uibuaji, utekelezaji, uendeshaji na matunzo ya skimu zao za umwagiliaji na kupanga mapema namna ya kutunza skimu hizo kabla hazijajengwa.

Naye Mshauri wa JICA nchini, Namiko Yamada amesema kuwa kwa zaidi ya miaka 40 serikali ya Japan imetoa misaada kusaidia maendelea ya kilimo hususani kilimo cha umwagiliaji, ambapo amesema kuwa JICA chini ya mradi wa TANCAID II imeweza kusaidia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji na kutoa mafunzo kwa vyama vya wamwagiliaji na wahandisi wa umwagiliaji.

 

Viongozi Simiyu wapingana hadharani, mmoja atoa maagizo, mwingine atengua
Rais Magufuli atoa ujumbe kwa bara la Afrika, 'Hakuna lisilowezekana'