Wakandarasi wa Kampuni za CHICCO Engineering na Nyanza Road Work waliokamatwa Oktoba 24, 2019 na Jeshi la Polisi Kanda maalumu ya Dar es salaam kwa agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda wameachiwa kwa dhamana leo Oktoba 25, 2019.

Wakandarasi hao walikamatwa kwa kosa la Kushindwa kutekeleza miradi ya Ujenzi wa mto Ng’ombe na barabara ya Kivule kwa wakati na kuleta usumbufu mkubwa kwa wananchi ukiwemo wa mafuriko, nyumba Kubomoka, uharibifu wa mali, ajali na magari kuharibika huku wakandarasi hao wakila maisha mitaani.

Wamepewa dhamana hiyo leo na kutakiwa kwenda moja kwa moja katika maeneo ya kazi kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katibu tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge amesema licha kupewa fedha, wameshindwa kutekeleza kazi waliyopewa.

Jumanne Oktoba 22, 2019 Makonda alitangaza kuwapa siku tano makandarasi wanaosuasua kutekeleza miradi waliyopewa akitishia kuwakamata na kuwafukuza endapo hawatabadilika.

Leo Makonda amethibitisha Wakandarasi hao kuachiwa kwa dhamana akiwataka kwenda moja kwa moja kwenye maeneo yao ya kazi.

“Tumewapa dhamana ili wakafanye kazi. Tunataka kazi ifanyike, wenyewe wametuhakikishia kuwa wataongeza vifaa na ajira ili kazi ikamilike ndani ya miezi 10 badala ya 18 waliyopanga awali,” amesema Makonda.

Wakandarasi wa kampuni ya Nyanza Road Work wao wanajenga barabara ya Banana –Kitunda na Chicco Engineering wanajenga daraja la Mto Ngo’mbe.

Tanzania yaipigania Zimbabwe, yataka dunia iiondolee vikwazo bila masharti
Watatu kizimbani kwa wizi wa tausi watatu wa Ikulu