Naibu Waziri wa Maji na Mbunge wa Jimbo la Pangani, Jumaa Aweso amewataka wahandisi wasiokuwa na sifa na vigezo ndani ya wizara hiyo hususani wahandisi wababaishaji, kujitathimini mapema kwani msasa utapita kwa ajili yao.

Aweso ametoa tamko hilo akiwa Mkoani Kagera katika ziara mahususi iliyoanzia katika ofisi za mamlaka ya maji safi na maji taka mjini Bukoba (BUWASA), kisha kutembelea kituo cha uzalishaji maji kilichopo Bunena, Bukoba Manispaa na baadaye kukagua tanki la maji lililopo Kashura na lile linalojengwa Ihungo ndani ya Manispaa ya Bukoba.

Katika ziara hiyo akiambatana na Mstahiki Meya wa manispaa hiyo, Chief Kalumuna, Mkurugenzi wa maji (BUWASA), wahandisi na wataalamu wa Idara hiyo, Naibu Waziri amefurahishwa na kukamilika kwa mradi huo wa maji mjini Bukoba uliogharimu pesa nyingi, wenye uwezo wa kuzalisha lita za maji zaidi ya Milioni 18 wakati mahitaji ya wakazi wa manispaa ya Bukoba ni lita Milioni 13.

Licha ya kukamilika kwa mradi huo kuna baadhi ya maeneo hawajafikiwa na huduma hiyo muhimu ya maji, bado maeneo ambayo mpaka sasa hayajafikiwa na mradi huo ni pamoja na Buhembe, Nyanga, Nshambya, Kahororo, Ijuganyondo na Kibeta, na hivyo Naibu Waziri amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Maji kushughulikia suala hilo kwa karibu ili kufikia malengo yaliyowekwa ambayo ni kila mwananchi kupata Huduma ya maji safi na salama kwa karibu.

Sambamba na hayo Wananchi wametakiwa kuendelea kutunza na kulinda vyanzo vya maji ikiwemo miundo mbinu ya maji ili iendelee kuwanufaisha katika maisha ya kila siku, ambapo asilimia kubwa hutegemea maji kwa matumizi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kulipia Ankara zao za maji pasipo kususbiri hadi kukatiwa huduma.

Awesso yupo Mkoani Kagera katika ziara ya kikazi na anategemea kutembelea wilaya zote akiwa tayari amehitimisha ziara yake Bukoba Manispaa.

Tume ya Uchaguzi Congo DR yaivimbia UN 'Tunamaamuzi yetu'
LIVE: Rais Magufuli akihutubia baada ya ndege nyingine ya Tanzania kuwasili