Watu wawili wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi ya Kisutu jijini Dar es Salaam kwa makosa ya kutengeneza tovuti na akaunti bandia za watu mbalimbali ikiwa ni pamoja na jina la rais Jakaya Kikwete.

Washtakiwa hao waliotajwa kwa jina la Maximilian Raphael Msaki na Patrick James Natala, wanakabiliwa na mashitaka kumi ikiwa ni pamoja na kujipatia fedha kwa udanganyifu.

Imeelezwa kuwa washtakiwa hao walitumia tovuti na akaunti za mitandao zenye majina Rais Jakaya Kikwete Foundation, TCRA foundation, Ridhiwani Social Company na makampuni ya mikopo yenye majina ya Zitto Kabwe Foundation, Hisa Tanzania, Akiba Saccos na mengine. Watuhumiwa hao wanadaiwa kuzitumia akaunti hizo kujipatia fedha kinyume cha sherika kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2015.

Washtakiwa hao pia wanadaiwa kugushi vyeti vya vyuo vikuu mbalimbali nchini pamoja na vyeti vya elimu ya sekondari kwa lengo la kufanya utapeli kinyume na sheria ya makosa ya jinai.

Hata hivyo, watuhumiwa hao walikana mashtaka waliyosomewa mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama ya Kisutu, Emilius Mchauru na kurudishwa rumande hadi kesi hiyo itakaposomwa tena tarehe 24 mwezi huu.

Tanzia: Mgombea Ubunge Afariki
Lowassa Aeleza Atakapotoa Fedha Za Kutekeleza Ahadi Zake