Wabunge nchini Somalia wamewasilisha bungeni azimio la kutaka kumpigia kura ya kutokuwa na imani kwa lengo la kumng’oa madarakani Rais wa nchi hiyo, Mohammed ‘Farmajo’ Abdullahi.

Kwa mujibu wa Reuters ambao wameiona nakala ya azimio hilo, sababu zilizoanishwa ni pamoja na kumtuhumu Rais huyo kuwa amesaini kwa siri mikataba na nchi za Ethiopia na Eritrea. Imeelezwa kuwa mikataba hiyo inahusu kuziruhusu nchi hizo kutumia bandari ya nchi hiyo pamoja na masuala mengine ya kiusalama.

Rais wa Somalia, Mohammed ‘Farmajo’ Abdullahi

“Ni kweli sisi wabunge tumewasilisha rasmi azimio la kumpigia kura ya kutokuwa na imani Rais wa Somalia,” Abdikarim H.Abd Buh, Mbunge na mwanasiasa mwandamizi nchini humo amekaririwa na Reuters.

Hata hivyo, Naibu Spika wa Bunge ametupilia mbali hoja hiyo iliyowasilishwa akieleza kuwa haina mashiko bali inalenga kusababisha sintofahamu na taharuki za kisiasa zisizo za msingi.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Somalia, mapema leo kulikuwa na makundi ya waandamanaji wanaopinga hoja hiyo ya wabunge wa kambi ya upinzani.

Kikatiba, wabunge 92 kati ya 275 walitakiwa kutia saini hoja hiyo ili iweze kuwasilishwa rasmi bungeni. Hata hivyo, kiti cha naibu spika tayari kimeshaiweka kando hoja hiyo hata kabla ya kupitia mchakato huo.

Rais Farmajo aliingia madarakani mwaka 2017 akiwa ni Rais wa tisa wa nchi hiyo. Kabla ya kushika nafasi hiyo ya juu, alikuwa Waziri Mkuu tangu mwaka 2010 hadi 2011.

Video: Ni hatari sana tusipowabana viongozi wetu- Wakili Manyama
Serikali kula sahani moja na viongozi wasiokuwa waadilifu