Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amewatahadharisha waangalizi wa uchaguzi mkuu takribani 600 kutoka mataifa mbalimbali duniani kutoingilia mchakato wa uchaguzi.

Tahadhari hiyo imetolewa na waziri huyo wa mambo ya nje katika mkutano wake na Mabalozi wa nchi mbalimbali uliohudhuriwa pia na waandishi wa habari.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe

Membe aliwataka waangalizi hao kuhakikisha wanafuata taratibu na sheria za uangalizi wa chaguzi na kutoshiriki katika kufanya kazi ambazo zinapaswa kufanywa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) ikiwa ni pamoja na kutangaza matokeo kwa hali yoyote ile.

Aidha amewataka wasimamizi hao kuhakikisha hawajihusishi na harakati za kisiasa kwa kwa kuunga mkono chama chochote cha kisiasa.

“Serikali imejikita katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu,” Membe alisema. “Tumejidhatiti katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uhuru na haki ili matakwa ya wananchi yazingatiwe,” aliongeza.

Alibainisha kuwa waangalizi hao wanatarajiwa kutoka mataifa mbalimbali yakiwemo Marekani, Uingereza, Umoja wa nchi za Ulaya pamoja na Jumuiya nyingine za Afrika.

Uchaguzi mkuu wa mwaka huu umevuta umakini wa dunia kutokana na msisimko wa ushindani mkubwa uliopo hususan kati ya chama tawala (CCM) kilichomsimamisha Dk John Magufuli kugombea urais,  na Chadema iliyomsimamisha Edward Lowassa anayeungwa mkono na vyama vinne vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Waangalizi kati ya 600 hadi 900 wa kimataifa wanatarajiwa kushuhudia kinachoendelea katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Uchaguzi wa mwaka 2010, ulishuhudiwa na waangalizi 500 kutoka nje ya nchi.

Magufuli Afananisha Mabadiliko Ya Haraka Na Machafuko Ya Kenya
Magufuli Aunga Mkono Wazo Maarufu La Lowassa