Ripoti ya Baraza la Umoja wa Ulaya kuhusu uhuru wa vyombo vya habari imeonyesha kuwa mwaka 2018 ulikuwa mwaka mbaya zaidi kwa waandishi wa habari barani humo tangu kumalizika kwa vita baridi.

Ripoti hiyo iliyopewa kichwa cha habari Demokrasia hatarini, imebaini  kuwa uhuru wa vyombo vya habari katika nchi wanachama uko katika hali mbaya tangu kumalizika kwa vita baridi.

Aidha, ripoti hiyo iliyotolewa kwa ushirikiano na Jukwaa la ulinzi na usalama wa waandishi wa habari, imesema kuwa mashambulizi dhidi ya wanataaluma wa habari yameongezeka maradufu katika kipindi cha miaka michache iliyopita.

Waandishi wa habari wawili waliuawa mwaka 2018 kuhusiana na kazi zao, akiwemo Jan Kuciak wa Slovakia pamoja na Jamal Khashoggi ambaye kifo chake katika ubalozi wa Saudi Arabia jijini Istanbul bado kinachungzwa, huku Jukwaa hilo likipokea taarifa za mashambulizi mengine kadhaa ikiwa ni pamoja na mabomu ya kwenye magari, shambulio la visu, uchomaji wa mali na uvamizi wa ofisi za magazeti.

Mashambulizi yaliyotajwa katika ripoti hiyo barani Ulaya ni pamoja na kauli zilizotolewa na viongozi wa siasa zikiwemo za wale waliosema wanasikitika kwamba bado waandishi wa habari hawajatoweka kabisa duniani na hata kutoa orodha ya waandishi wa habari ambao walidiriki kukosoa serikali na kuwaita wasaliti.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo waandishi wa habari 130 bado walikuwa kizuizini hadi kufikia Desemba 31 mwaka jana wengi ni kutoka nchini Uturuki. nchi hiyo imesalia kuwa taifa lenye idadi kubwa duniani lenye waandishi wa habari walioko gerezani, ambapo zaidi ya waandishi 200 walikamatwa tangu kushindwa kwa jaribio la mapinduzi mnamo mwaka 2016.

Hata hivyo, ripoti hiyo imekosoa utamaduni wa kushindwa kwa mamlaka za serikali katika kuwatambua, kuwashitaki na kuwaadhibu wale wote wanaohusika na uhalifu wa vurugu dhidi ya waandishi. ambapo nchi 47 wanachama wa Baraza hilo waliahidi kuchukua hatua za kukomesha kinga mwaka 2016 lakini hakuna hatua iliyopigwa.

Mpelelezi nguli wa jeshi la Marekani ageuka, aisaidia Iran
Wodi ya Wazazi Hospitali ya Mpwapwa yazidiwa na Wagonjwa