Waandamanaji katika mji wa Beni, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wamechoma kambi ya jeshi ya Umoja wa Mataifa kwa madai kuwa imeshindwa kuzuia mashambulizi ya kundi la kigaidi la Allied Democratic Forces (ADF).

Waandamanaji hao walichukua hatua hiyo baada ya ADF  kuvamia mji huo Jumapili usiku na kuua watu wanane na kujeruhi makumi, huku wakifanya vitendo vingine vya kinyama.

Jana, waandamanaji walifika katika kambi ya Umoja wa Mataifa inayojulikana zaidi kwa jina la Monusco, na wakafanya fujo ikiwa ni pamoja na kuchoma majengo ya ofisi.

“Ofisi kadhaa za makao makuu ya Monusco zilichomwa moto na kuharibiwa vibaya,” kiongozi wa jamii ya watu wa Beni, Teddy Kataliko aliiambia Reuters.

“Wakaazi wa eneo hilo wanataka Munosco iondoke mjini Beni kwa sababu haina faida kwao na imeshindwa kufanya kazi ya kuwalinda,” aliongeza.

Pia, waandamanaji walivamia ofisi ya Meya wa Beni na kuichoma moto, kwa mujibu wa tweet ya jeshi la polisi iliyoandikwa kwa lugha ya Kifaransa.

Umoja wa Mataifa una wanajeshi 18,000 nchini humo, lakini wanajeshi hao kwa kushirikiana na jeshi la nchi hiyo wamekuwa wakipambana bila mafanikio ya kudumu dhidi ya makundi ya kigaidi na makundi ya waasi.

Kundi la ADF ni moja kati ya makundi ya kigaidi yanayofanya shughuli zake katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kundi hilo lilianzishwa na waasi wa jeshi la Uganda.

Napol yaandaliwa Salah
Video: Jafo amaliza mchezo serikali za mitaa, Msako TRA nyumba kwa nyumba