Askari Polisi wa Kikosi cha Kuzuia ghasia nchini Hispania amefariki dunia baada ya vurugu kuzuka mitaani usiku wa kuamkia leo, zikihusisha mashabiki wa Timu za Spartak Moscow ya Urusi na Athletic Bilbao kabla ya mechi ya Ligi ya Europa baina ya timu hizo.

Askari huyo alifariki dunia hospitalini baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo baada ya kupata shinikizo la damu, wakati wakizuia ghasia baina ya mashabiki wa timu hizo mbili.

Katika tukio hilo ambalo liliambatana pia na kurushiana mioto, vipeperushi na chupa baina ya mashabiki, watu zaidi ya watano walikamatwa baada ya vurugu huku wengi wao wakijeruhiwa na kukimbizwa hospitali.

Mashabiki wapatao 2,500 wa Urusi walitarajiwa kusafiri kwenda Hispania kwenye mechi hiyo hali iliyosababisha ulinzi mkubwa ambao hata hivyo haukutosha kuzuia vurugu zilizojitokeza.

Kiasi cha askari polisi 700 na walinzi wengine 200 wa kampuni binafsi inaelezwa walikuwa mjini Bilbao na Uwanja wa San Mames kujaribu kuzuia vurugu.

Katika mchezo huo Spartak imetolewa kwenye Europa League licha ya kushinda 2-1, kufuatia kufungwa 3-1 katika mechi ya kwanza iliyopigwa nchini Urusi.

Chama cha Soka barani Ulaya (UEFA) kimelaani tukio hilo na kusema “Tunawasiliana na mamlaka za pale kupata maelezo zaidi juu ya kilichotokea. UEFA inatuma salamu za rambirambi kwa familia na jamaa wa Afisa Polisi aliyefariki dunia,”.

Video: JPM, Kenyatta wasema wapo sawa, wawaagiza mawaziri kutatua tofauti ndogondogo zilizopo
Serengeti Boys kushiriki mashindano ya CAF-Cecafa Cup