Mameneja wa klabu za ligi kuu ya soka nchini Uingereza jana walikutana katika kikao maalum cha kujiandaa na msimu mpya wa ligi, ambao utaanza mwishoni mwa juma hili kwa michezo kumi kuchezwa.

Mameneja hao walikutana jijini London kujadili masuala mbali mbali kupitia umoja wao, na inaaminika maamuzi yaliyofikiwa katika kikao hicho yatafanyiwa kazi katika msimu mzima wa ligi ambao utafikia kikomo mwezi May mwaka 2015.

Wakati wakiwasili tayari kwa mkutano huo, mameneja wote walioneka kuwa na furaha huku wakiwasalimu waandishi wa habari ambao walijitokeza kwa lengo la kuangalia majukumu yao ya kikazi.

Hata hivyo, kituko ambacho kinadhaniwa kilijiri ndani ya ukumbi wa mkutano ni kukutana tena kwa meneja wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger na Jose Mourinho wa klabu ya Chelsea, ambao siku tatu zilizopita walishindwa kusalimiana kutokana na chokochoko zinazoendelea baina yao.

Nje ya ukumbi  Arsene Wenger alisalimiana na kila mtu huku akiwa sanjari na meneja wa Manchester United, Louis van Gaal hali ambayo ilielezea mahusiano mazuri kati ya wawili hao.

Meneja wa Spurs, Mauricio Pochettino hakuhudhuria mkutano huo, kufuatia majukumu yanayomkabili kwa sasa ya kukisimamia kikosi chake, ambacho kipo nchini Ujerumani kikishiriki michuano ya kombe la Audi ambayo mwenyeji wake ni FC Bayern Munich.

Mameneja wa klabu za Watford, Norwich City pamoja na Bournemouth, Eddie Howe, Alex Neil na Quique Sanchez Flores walikuwa wakiingia katika mkutano huo kwa mara ya kwanza kufuatia klabu zao kupanda daraja.

Katika hatua nyingine meneja wa klabu ya Leicester City, Claudio Ranieri alihudhuria mkutano huo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 12 kupita, ambayo ilishuhudia akiwa na kikosi cha Chelsea kabla ya kumkabidhi kijiti Jose Mourinho mwaka 2004.

 

Kakobe Arusha Jiwe Kwa Wagombea Urais
Nightclub Aliyokuwamo Drake Yashambuliwa Kwa Risasi, Wawili Wauwa