Viongozi wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye na Mbunge Robert Kyagulani maarufu Bobi Wine, wamekubaliana kufanya kazi kwa pamoja ili kukishinda chama kilichopo madarakani cha NRM cha Rais Yoweri Museveni kwenye uchaguzi wa mwaka 2021.

Taarifa hiyo imetolewa kwa vyombo vya habari na wasemaji wa vuguvugu la wanaharakati wa makundi ya People’s Power la Bobi Wine na la People’s government la Besigye.

Wakizungumza na vyombo vya habari jijini Kampala, msemaji wa People’s Power, Joel Ssenyonyi na msemaji wa vuguvugu la mapinduzi People’s government la Kizza Besigye, Mbunge Betty Nambooze wamesema kuwa pande mbili za vuguvugu hilo zitafanya harakati za pamoja ili kumzuia Rais Museveni aliyepo madarakani tangu mwaka 1986 asishinde uchaguzi wa 2021.

“Makundi mawili haya yana shughuli tofauti na tutaendelea kuzifanyia kazi na mara kwa mara tutafanya shughuli za pamoja”, amesema Ssenyonyi, msemaji wa People’s power inayoongozwa na Bobi Wine.

Bobi Wine alikiri kwamba vuguvugu lake limekuwa likifanya mikutano na vyama tofauti tofauti vya siasa wakiwemo wapinzani wa ndani ya chama tawala cha NRM cha Yoweri Museveni na chama cha Kizza Besigye.

Mbunge Betty Nambooze amesema kuwa katika mikutano kati ya wapinzani wa Rais Museveni, suala la kuwa na mgombea moja kwenye uchaguzi ujao lilijadiliwa, na lengo hasa ni kurejesha utawala unaoheshimu uhuru wa wanainchi wote wa Uganda.

Aidha, Nambooze ameongeza kuwa, lengo kuu ni kumuondoa rais Museveni hata kabla ya uchaguzi wa 2021, na iwapo mpambano huo utahitaji kuwa na mgombea mmoja atakaewakilisha upinzani ili ufikie lengo hilo basi wapinzani hawatokua na budi kumteua mgombea mmoja.

Kwa upande wake Mchambuzi wa siasa za Uganda, Akol Amazima amesema kuwa kuungana kwa Besigye na Bobi Wine bila shaka, kutampa changamoto kubwa rais Museveni.

Mzee Mengi hakuwa mbaguzi kwa wanasiasa- Nape Nnauye
Video: Mambo 10 usiyofahamu kuhusu mapacha